Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu
wake Mahmoud Mgimwa wakimsikiliza kwa makini Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani
wa wizara hiyo, Mchungaji Peter Msigwa alipokuwa akitoa CD bungeni aliyodai
inaonyesha moja ya kampuni inayofanya uwindaji haramu kwenye baadhi ya mbuga za
wanyama nchini. Picha na Edwin Mjwahuzi.
Dodoma.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema Wizara
ya Maliasili na Utalii inaongozwa kwa ubabaishaji na ‘mvutano wa kimasilahi’
baina ya waziri na katibu mkuu, hivyo kukwamisha shughuli za kuendeleza utalii.
Msemaji wa kambi hiyo
(Maliasili na Utalii), Mchungaji Peter Msigwa alitoa kauli hiyo juzi wakati
akisoma maoni kuhusu hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa wizara hiyo
kwa mwaka 2014/15.
Alisema kambi ya upinzani inasikitishwa na
mvutano baina ya Waziri Lazaro Nyalandu na Katibu Mkuu wake, Maimuna Tarishi
ambao unaonyesha udhaifu wa Serikali.
“Hii inathibitisha kuwa
Serikali ni dhaifu kwa kuwa, waziri na katibu mkuu wa wizara moja wanafanya kazi
bila kushirikiana na kila mmoja anaonekana kumvizia mwenzake hadharani badala ya
kukaa kwa pamoja kutekeleza maazimio ya Bunge,” alisema Msigwa.
Alisema kitendo cha Waziri Nyalandu kuwasimamisha kazi wakurugenzi
wawili, lakini wakarudishwa na katibu mkuu huku akisema taratibu za kuwafukuza
hazikufuatwa na hii ni dalili kuwa hata yeye (Nyalandu) siyo msafi kwa kuwa
anashindwa hata kujua mipaka yake ya kazi.
Mbali na mvutano huo,
Msigwa alisema maazimio ya Bunge kuhusu matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili
yanaendelea kupuuzwa na watumishi wenye tuhuma wakihamishwa vitengo.
“Ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote hamfichi mnafiki
na debe tupu haliachi kutika (siyo maneno yangu, bali ya wahenga). Siyo mara ya
kwanza kambi ya upinzani kuhoji juu ya usafi wa Lazaro Nyalandu,” alisema.
Alisema Waziri Nyalandu alipozungumza katika kikao cha wadau wa
ulinzi wa maliasili Juni mwaka jana mkoani Iringa, aliahidi kuwa majina ya
majangili yakiwamo ya vigogo yangetangazwa hadharani, lakini hadi sasa hakuna
majina yoyote yaliyotangazwa hadharani.
Uteuzi wa Sarakikya
Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) alizungumzia
kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Paul Sarakikya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi
wa Wanyamapori, jambo alilosema ni kinyume na haki za binadamu.
Msemaji huyo alibainisha kuwa, wakati wote Watanzania wanajiuliza
maswali ambayo hayajapata majibu kuhusu vigezo vilivyotumika kumteua Sarakikya.
“Katika Operesheni Tokomeza, mtu huyu alikuwa kiongozi wa
utekelezaji wa moja kwa moja na kinachodaiwa ni uvunjifu wa haki za binadamu,
inashangaza kuona mtu huyu tena ndiye ana nafasi ya kukaimu ukurugenzi, lini
kawa msafi?” alihoji Msigwa.MWANANCHI (TK).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni