Ijumaa, 23 Mei 2014
MTOTO ALIYEISHI KWENYE BOX MIAKA MINNE MIFUPA YAKE IMEATHIRIKIA
POLISI mkoani Morogoro, inaendelea kuchungua kilichotokea mpaka mtoto mkoani hapa (jina limehifadhiwa), akateswa na mzazi mlezi kwa kuwekwa katika boksi tangu akiwa na miezi tisa, mpaka alipotimiza miaka minne. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, amesema, baba mzazi wa mtoto huyo, jina tunalo ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro alitakiwa kwenda kutoa maelezo kituoni leolakini hakutokea.
Kamanda Paul alisema jana kuwa, walimtafuta mzazi huyo kwa simu ili kumkumbusha umuhimu wa kufika Polisi kutoa maelezo, lakini simu zake zilikuwa zimezimwa.
Gazeti hili lilifika kwa mwajiri wake katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ambako hakuwepo kwa kuwa aliaga kwamba amekwenda katika Kituo cha Ustawi wa Jamii, alikodai kuwa aliitwa.
Hata hivyo, gazeti hili lilipofika katika ofisi hiyo, lilihakikishiwa na Ofisa Ustawi wa Jamii, Oswin Ngungamtitu, kuwa mtuhumiwa hakuwa amefika katika eneo hilo, wala hakukuwa na mwito wa yeye kufika katika ofisi hiyo.
Katika tukio lingine la kutia shaka, gazeti hili lilipohojiana na Mtuhumiwa katika nyakati tofauti juzi, alitoa taarifa mbili tofauti, kuhusu sababu za kumuacha mwanaye kwa mama mkubwa wake, Mariam Said, aliyemuweka katika boksi kwa zaidi ya miaka mitatu.
Katika mahojiano ya awali, alidai baada ya mzazi mwenzake, Mwasiti Ramadhan kufariki dunia, alishindwa kumchukua mtoto wake kwa sababu tayari alishakuwa na mke.
Alidai kwa kuwa alikuwa ameoa, alikubaliana na upande wa pili wa familia ya marehemu, kuwa mwanaye huyo alelewe na mama yake mkubwa, Mariamu.
Katika mahojiano na mwandishi mwingine wa gazeti hili juzi hiyo hiyo, alidai mwanae huyo alichukuliwa na Mama yake mkubwa ili kumlea akiwa na umri ndogo na mara zote alikuwa akipeleka fedha za matumizi.
Alidai kwa mara ya mwisho alimwona mwanae huyo miezi miwili iliyopita akiwa na afya ya kuridhisha, wakati taarifa zilizotolewa na Mariam, zilidai kuwa mtoto huyo hajaogeshwa tangu Julai mwaka jana.
“ Kila nikienda kumwona nyumbani kwao sikubahatika kumwona , nilikuwa nikiambiwa amelala ama ametoka na watoto wenzake...isipokuwa miezi miwili iliyopita,” alidai Rashid kauli inayoonesha kuwa mtoto huyo alikuwa akitoka na wenzake wakati majirani walitoa ushahidi kuwa hawakuwahi kufahamu uwepo wa mtoto katika nyumba hiyo.
Taarifa kutoka katika Hospitali ya Rufaa mkoani Morogoro, zimeeleza kuwa baada ya uchunguzi wa awali wa afya ya mtoto huyo, alibainika kuwa na niumonia, ulegevu wa viungo ikiwa ni pamoja na baadhi ya mifupa katika mwili wake kuvunjika.
Daktari Bingwa wa watoto, Dr Hores Msaky alipozungumza na gazeti hili jana, alisema walimpokea mtoto huyo juzi alikuwa katika hali ya uchafu usio wa kawaida.
Msaky alisema waliamua kumfanyia vipimo vya awali pamoja na picha za X ray, wakagundua kuwa mifupa yake si ya kawaida, inaonekana imevunjika ingawa hawajajua nini kimemvunja.
“Tunachokifanya hivi sasa ni kujaribu kujua tatizo hilo limetokana na nini,” alisema daktari huyo. Hata hivyo Dr Msaky alisema kuwa hospitali hiyo haina vifaa vingi vya kupimia mifupa, hivyo imeshauriwa apelekwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi .
Mwandishi wa habari hizi alifanikiwa kuingia wodi aliyolazwa mtoto huyo na kumkuta akiwa amechangamka, na alipoulizwa anaendeleaje alisema anasikia maumivu katika sehemu ya kifua .
Mtoto huyo alikuwa akidhulumiwa haki yake ya utu na kuteswa kwa zaidi ya miaka mitatu, kwa kufungiwa ndani ya boksi kama mnyama, ili asiamumbukize mama mlezi virusi vinavyosababisha UKIMWI.
Unyama huo wa kusikitisha, ulikuwa ukifanyika muda wote huo kwa mtoto huyo Morogoro mjini katika mtaa wa Azimio bila kuripotiwa popote, huku wakazi na majirani wa nyumba hiyo wakisikia akikohoa na kulia usiku, na baba yake mzazi akiendelea na maisha kwa kumuogopa mkewe. Wakizungumza na gazeti hili juzi majirani hao walidai Mariam alihamia katika nyumba hiyo mwaka 2010, lakini hawakuwahi kumuona akiwa na mtoto.
Hata hivyo majirani hao walikiri kwamba walikuwa wakisikia mtoto akikohoa na kulia hasa nyakati za usiku, lakini walikuwa na wasiwasi kuwa huenda mtuhumiwa alikuwa mshirikina anayefuga watu waliouawa kishirikina au kwa jina lingine misukule.
Hatimaye juzi mateso ya mtoto huyo yalipungua, baada ya msamaria mmoja kupata taarifa sahihi, kwamba ndani ya nyumba hiyo kuna kiumbe asiye na hatia aliye katika mateso na kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo.
Zongo akiwa katika kazi za kawaida katika mtaa huo, alipata taarifa kutoka kwa majirani kuwa kuna mwanamke, Mariamu Said, amemficha mtoto ndani ya boksi na hamfanyii usafi wala kumtoa nje.
Baada ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta mwenyeji wake, Mwenyekiti wa mtaa huo, Tatu Mgagalana na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo ambapo walimkuta mtuhumiwa, Mariamu na kuanza kumuhoji kuhusu tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa Zongo, wakati mtuhumiwa akijibu maswali aliyoulizwa huku akibabaika, ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa hali iliyowapa wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa Mariamu kwa nguvu, hatua iliyomuokoa mtoto huyo kutoka katika mateso ya zaidi ya miaka mitatu.
Ofisa huyo na mwenyeji wake walimkuta mtoto huyo ametapakaa uchafu uliotokana na kinyesi na mkojo, kwa kuwa boksi hilo lilikuwa chumba chake cha kulala, meza yake ya chakula na maji na choo kwa ajili ya haja ndogo na kubwa.HABARILEO
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni