Watu wawili wamejeruhiwa katika mlipuko uliotokea mjini Mombasa pwani ya
Kenya.
Miongoni mwa wawili hao ni afisa wa polisi aliyekimbizwa katika hospitali ya
mkoa kupokea matibabu.
Shambulio hilo lilitokea wakati maafisa wa polisi walipomkamata mshukiwa wa
ugaidi, na hapo pakatokea mtu wa pili aliyewarushia guruneti katika jitihada ya
kumuokoa mshukiwa aliyekamatwa na alifanikiwa kuondoka naye huku akimwacha polisi na mjeraha ya bomu na kumpiga risasi moja makalioni.
Mbunge wa Mvita kutoka eneo hilo, Abdulswamad Sharrif ambaye ni miongoni mwa
viongozi waliofika katika eneo hilo punde baada ya mlipuko huo, amelaumu udhaifu
katika idara ya ujasusi Kenya kwa kutoweza kutambua mipango ya mashambulio kama
hayo kabla ya yafanyike, ili kuweza kuyatibua.
Akizungumza na BBC Abdulswamad amesema, 'Ni lazima tuweze kukubali kasoro iko
wapi, ili tuweze kujua suluhisho litakuja vipi'.
Shabulio hilo limetokea wakati usalama umeimarishwa nchini Kenya kutokana na
tisho la kutokea shambulio la kigaidi dhidi ya maeneo ya umma.
Katika siku za hivi karibuni Kenya imekuwa ikikabiliwa na mashambulio kadhaa
katika maeneo mbali mbali nchini ukiwemo mji huo wa Mombasa na Nairobi,
yaliosababisha vifo vya watu kadhaa na wengine wengi kujeruhiwa.
Ni hivi juzi tu watu 10 waliuawa huku zaidi ya hamsini walijeruhiwa katika
milipuko miwili iliotokea katika Soko kubwa la nguo la Gikomba katika mji mkuu
Nairobi.(TK)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni