Polisi katika wilaya ya Bukoba nchini Tanzania imemkamata baba kwa
tuhuma za kumfungia na kumwadhibu mwanae mwenye umri wa miaka sita kwa muda wa
miezi saba ndani bila kutoka nje.
Kwa mujibu wa afisa mtendaji wa eneo hilo, mtoto huyo ana makovu ya kupigwa mwili mzima ambayo hata baada ya miezi sita hayawezi kufutika.
Mtoto huyo ameyapata masaibu hayo kwa madai kwamba haendi haja chooni.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Bwizanduru, Edward Muhezi anasema Emmanuel Justinian aliamua kumfungia ndani mwanawe Erick Emmanuel kwa muda wa miezi saba bila kuona jua huku akimcharaza viboko.
Inaidaiwa kwamba kushindwa kwa mtoto huyo kutojisaidia chooni kulimkera babake na hatimaye aliamua kumfungia kwa muda wote huo na kumcharaza viboko ambayo inasemekana vimemsababishia maumivu makali Erick.
"Mtoto amezidiwa sana na ana majeraha makali, bado yupo hospitalini na tunasubiri ripoti ya madaktari," alisema Edward Muhezi.
Awali afisa huyo alielezewa kwamba mtoto huyo anasoma, lakini baada ya uchunguzi na kuwasiliana na majirani katika eneo hilo, anasema waligundua kwamba mtoto huyo amekuwa akiteswa na hasomi.
Kwa mujibu wa uongozi wa serikali ya mtaa ya eneo hilo, mzazi huyo anatarajiwa kufikishwa kizimbani wakati wowote kuanzia sasa ili kujibu tuhuma za ukatili dhidi ya mtoto baada ya ripoti ya madaktari kutolewa.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa visa vya ukatili dhidi ya watoto kuripotiwa.
Kumekuwa na matukio mbali mbali yanayogusa nyoyo za wengi huku la hivi karibuni zaidi likiwa ni lile la mtoto Nasra aliyefariki dunia baada ya kuwekwa kwenye boksi kwa muda wa miaka zaidi ya 3 (TK)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni