Ijumaa, 27 Juni 2014

JAJI WEREMA VS Mhe KAFULILA NANI KUIBUKA MSHINDI?


Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu (kushoto) akijaribu kuwasuluhisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kulia) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila katika Viwanja vya Bunge Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi.

Dodoma.

Mvutano kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila umechukua sura mpya baada ya mwanasheria huyo kugoma kupatanishwa huku akitishia ‘kumshughulikia’ mbunge huyo.
Ugomvi baina yao uliendelea jana asubuhi nje ya Ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha kikao cha Bunge hadi leo.


Licha ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kumwita Jaji Werema na Kafulila akiwataka kupeana mikono kama ishara ya kuzika tofauti zao, Jaji Werema alikataa na nusura amvamie mbunge huyo.


Juzi asubuhi baada ya Zungu kuahirisha kikao cha Bunge, muda mfupi baada ya Jaji Werema na Kafulila kurushiana maneno bungeni, mwanasheria huyo alitaka kumtia adabu Kafulila kwa kumwita mwizi.


Kafulila alimwita Jaji Werema mwizi akijibu mapigo baada ya awali kuitwa tumbili na mwanasheria huyo.


Ilivyokuwa jana
Wakati akizungumza na gazeti hili mara baada ya Bunge kuahirishwa jana, Jaji Werema alikutana uso kwa uso na Kafulila katika Viwanja vya Bunge na kuanza kumlalamikia mbunge huyo kwa kitendo chake cha kumwita mwizi.


“Unamuona huyo jana (juzi), aliniita mimi mwizi. Yaani mtu mzima kama mimi naitwa mwizi, kwa kweli sikupendezwa kabisa na kauli yake,” alisema Jaji Werema huku akimfuata Kafulila ambaye alitembea harakaharaka kumkwepa mwanasheria huyo.


Jaji Werema alisema juzi alishikwa na jazba baada ya kuitwa mwizi lakini akasema hakuwa na nia ya kumpiga ndani ya Ukumbi wa Bunge.


Wakati Jaji Werema akiendelea kumlalamikia Kafulila, alitokea Zungu na kumtaka mwanasheria huyo kumsamehe mbunge huyo... “Mheshimiwa naomba mpeane tu mikono kama ishara ya kusameheana, yale mambo ya jana (juzi) yamekwisha.”


Lakini badala ya kukubaliana na ombi la Zungu, Jaji Werema alihamaki huku akitaka tena kumvamia Kafulila... “Mimi nakwambia Kafulila nitakukata kichwa, we subiri tu labda ukiniomba msamaha.”


Kafulila naye alijibu mapigo... “Huwezi kunikata kichwa Werema, huwezi, yaani uniue, hapana huwezi tena nakwambia huwezi.”


Wakati wakiendelea kurushiana maneno, Zungu alikuwa katikati yao, huku akiwasihi wapeane mkono na kusameheana bila mafanikio... “Haya mambo yamekwisha jamani, malizeni tofauti hizi.”


Kama vile alijua kuwa kauli ya kuua ilimchanganya Kafulila, Jaji Werema huku akitembea kuelekea katika Jengo la Utawala la Bunge alisema: “Siwezi kukuua kwa maana hiyo unayodhani, maana kufa utakufa kwa mapenzi ya Mungu, ila tutapambana tu, nitakuonyesha.”


Kauli ya Kafulila
Akizungumza baadaye, Kafulila alisema: “Kutokana na hali ilivyo sasa, nimeandika barua Ofisi ya Spika juu ya vitisho nilivyopewa na Jaji Werema, kwanza jana (juzi) alitaka kunivamia pale bungeni na kunipiga, leo (jana) asubuhi amenitishia kuwa atanikata kichwa.”


Kafulila alisema barua hiyo pia ataipeleka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa maelezo kuwa siku za hivi karibuni yamekuwa yakitokea matukio ya watu kutekwa, kuteswa na kutupwa porini... “Kwa nafasi yake, Werema anaweza kufanya lolote, hivyo barua hizo zinalenga kueleza alichokusudia kunifanyia.”


Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alipoulizwa kuhusu mvutano uliotokea juzi bungeni na barua za Kafulila alisema Ofisi ya Bunge haijapata malalamiko yoyote.


“Jana sikuwapo bungeni lakini mpaka sasa hakuna malalamiko yoyote yaliyoletwa katika Ofisi ya Bunge. Kama wangeshikana mashati ndani ya Bunge hilo lingekuwa kosa la kufanya fujo bungeni na adhabu zake zipo wazi,” alisema Joel.


Juzi, baada ya kurushiana maneno, Jaji Werema alinyanyuka alipokuwa amekaa na kuanza kumfuata Kafulila kabla ya kuzuiwa na kundi la mawaziri.


Mbali na kumzuia, mawaziri hao walimsindikiza hadi nje ya Ukumbi wa Bunge ambako alipanda gari lake na kuondoka.MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni