Makundi ya kigaidi na wanamgambo wamekuwa wakifaidi kutokana na
uwindaji haramu wenye thamani ya dola bilioni 213 kila mwaka, na kutishia
usalama wa kimataifa.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la UNEP.
Ripoti hiyo ilizinduliwa katika kongamano la kwanza kabisa la umoja wa
Mataifa kuhusu mazingira lililoandaliwa nchini Kenya
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kundi la Al Shabab nchini Somalia hupata kati ya
dola milioni 38 na 56 kila mwaka kutokana na biashara haramu ya uuzaji
mkaa.
Kwa jumla, makundi ya wanamgambo na kigaidi yaliyoko barani Afrika, yalipata
kati ya dola milioni 111 na 289 kila mwaka kwa kujishughulisha na kutoza ushuru
na uuzaji haramu wa mkaa.
“Makundi mengine yanayonufaika na biashara haramu ya wanyama pori
yalijipatia kati ya dola milioni 4 na 12.2 kila mwaka kutokana na uuzaji wa
pembe za ndovu katika eneo la Afrika ya Kati.
'Athari kwa idadi ya Ndovu'
Uhalifu huu pia ulichangia pakubwa katika kupunguka kwa idadi ya ndovu barani
Afrika,” ripoti hiyo ilisema.
Ripoti hiyo inajiri siku chache tuu baada ya BBC kushuhudia uharibifu mkubwa
wa mazingira katika mbuga ya wanyama ya Tsavo Mashariki.
BBC iliona mizoga ya ndovu waliouwawa hivi karibuni huku Kenya kwa mara
nyingine tena ikipoteza ndovu wake wanaoleta mapato mengi ya kitalii.
Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza anasema uvundo kutoka mzoga wa ndovu wa
miaka thelathini ulifuka kutoka umbali wa mita kadhaa kutoka eneo alipofia
Ndovu huyo baada ya kuuawa na wawindaji haramu
“Ndovu huyu alikuwa katika kundi la wengine watatu, na alipigwa risasi
kutumia bunduki ya rashasha na pembe zake kukatwa.
Tazama uso wake ulivyoharibiwa vibaya kwa kukatwakatwa,” alitueleza afisa
mmoja anayelinda mbuga ya kibinafsi katikati kabisa ya Mbuga za Tsavo Mashariki
na Magharibi.
Karibu na eneo hilo kulikuwa na alama nyingi nyeusi ardhini. Hii ilikuwa damu
ya ndovu wengine wawili waliouawa. Damu hiyo ilikuwa imekaukia ardhini na
kubadilika rangi kutokana na jua kali katika eneo hilo.
Uwindaji haramu umekuwa tatizo sugu katika mbuga ya wanyama ya Tsavo kutokana
na idadi kubwa ya ndovu katika eneo hilo. Hii imewavutia wawindaji haramu katika
eneo hilo.
'Kazi kukabiliana na wawindaji haramu'
“ Mwaka jana tulipoteza zaidi ya ndovu 70hapa, lakini mwaka huu pekee,
tayari tumeandikisha vifo vya ndovu zaidi ya 100. Hatujui hata idadi kamili
bado, ‘ alisema Dod Robson, mmiliki wa mbuga ya kibinafsi katika eneo la
Tsavo.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia masuala ya mazingira
UNEP inasema katika kipindi cha miaka tisa, idadi ya ndovu imepungua kwa kasi
kutokana na uwindaji haramu.
“Idadi ya ndovu wanaouawa kila mwaka sasa ni kati ya 20,000 na 25,000 na hii
ni katika idadi nzima ya kati ya ndovu 420,000 hadi 650,000, “ ilisema ripoti
hiyo iliyonzinduliwa jijini Nairobi.
“ Pembe za ndovu zinazotokana na uwindaji haramu barani Afrika na kuuzwa
barani Asia zina thamani ya kati ya dola milioni 165 na 188,” ripoti hiyo
iliendelea kufafanua
Asilimia 94 ya uwindaji haramu wa Vifaru unatokea nchini Zimbabwe na Afrika
Kusini, mataifa ambayo yana idadi kubwa zaidi ya Vifaru waliosalia duniani.
Ripoti hiyo sasa inapendekeza juhudi za pamoja za kimataifa kukabiliana na
uhalifu wa kimazingira zinahitajika haraka
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni