Polisi wametumia gesi ya kutoa machozi, kuwatawanya vijana
wenye hasira waliojaribu kuziba barabara muhimu mjini Mandera, Kaskazini mwa
Kenya , kupinga mauaji ya wahubiri wawili wa kiisilamu Jumapili usiku.
Waandamanaji waliwasha moto katika barabara zenye shughuli nyingi mjini humo
huku pakiwepo mchezo wa Paka na Panya kati ya vijana hao na polisi.Madai ambayo kamishna mkuu wa mji huo amekanusha akisema kuwa wahubiri hao walikuwa sehemu ya genge la watu watatu waliokuwa wanarejea kutoka nchini Somalia, ambako walikuwa wameenda kusaidia mpiganaji mmoja wa Al shabaab kuingia nchini Kenya.
Inadaiwa kuwa pia walikuwa wameenda kuchukua silaha usiku wa manane.
Kwa mujibu wa duru za usalama, wawili hao wanajulikana sana na waliwahi kuwashambulia polisi kwa maguruneti walipojaribu kusimamisha gari lao kwa ukaguzi.
Polisi wanasema kuwa walifanikiwa kupata maguruneti 8 kutoka kwa gari la washukiwa hao.
Kwa sasa polisi wanamsaka mshukiwa wa tatu ambaye wanasema alikuwa anajaribu kuingia nchini Kenya kimagendo. Alitoroka wakati wa tukio hilo.
Hali ya wasiwasi imetanda mjini humo. Polisi na wanajeshi wanashika doria katika mji huo unapakana na Somalia na ambao pia umeshuhudia mapigano ya kikabila.
Hivi karibuni watu 16 waliuawa wakati watu wa jamii mbili walipopigania rasilimali na wiki mbili zilizopita polisi wa Kenya waliuawa mpakani mwa Kenya na Somalia na tayari
Al shabaab wakiri kufanya mashambulizi hayo.
Kenya imeshuhudia visa kadhaa vya mashambulizi tangu mwaka 2011 wakati wanajeshi wake walipoingia kupambana na Al Shabaab(TK).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni