Alhamisi, 26 Juni 2014

WATOTO WAWILI WA FAMILIA MOJA WAFA KWA MOTO

Mtoto Dora Kaitaba (2) wakati wa uhai wake.
Watoto wawili wa familia moja, Nuru (3) na Dora Kaitaba (2), wamefariki dunia kwa kuungua moto baada ya moto mkubwa uliotokana na petroli kulipuka nyumbani kwao, Mapinga, Bagamoyo mkoani Pwani.Tukio hilo lililowaliza wengi, lilitokea saa tatu usiku, Jumapili iliyopita watoto hao wakiwa ndani na baba yao.
Kwa mujibu wa mashuhuda, baba mzazi wa watoto hao, Bwana Kaitaba ambaye ni mpiga picha wa kujitegemea, alikuwa amerejea kutoka Bunju B alikofuata petroli ambayo huiuza katika vipimo vidogo vya kwenye makopo ya maji nyumbani hapo.
Ilidaiwa kuwa alipofika kwake alishusha mzigo wa mafuta, watoto wake hao walikuwa wamelala katika kibanda chake cha biashara.
Mtoto Nuru Kaitaba (3) enzi za uhai wake.
Ghafla, mashuhuda wanasema, umeme ulikatika hali iliyomfanya Kaitaba kuchukua mshumaa na kuuwasha ili andelee na shughuli zake za kuhudumia wateja.
“Baada ya kuwasha mshumaa, moto huo ulidakwa na petroli hiyo iliyokuwa kwenye dumu na kusababisha mlipuko mkubwa.
Mama mzazi wa wa watoto hao (aliyenyosha mikono) akiwa na simanzi kwa kuwapoteza wanae.
Mashuhuda walisema Kaitaba alikimbia kutoka bandani, lakini alipopata akili ya kuwaokoa watoto wake tayari moto ulishakuwa mkubwa na hivyo kumfanya apige kelele za kuomba msaada.
Mchungaji akiziombea roho za marehemu hao, zikapate kupumzika kwa amani.
Hata hivyo, majirani walishindwa kuingia ndani kutokana na ukubwa wa moto huo na uduni wa vifaa vya kuzimia.
Watu wakiwa wanaangalia tukio hilo kwa masikitiko makubwa, Kikosi cha Zimamoto Bagamoyo kiliwasili kikiwa kimechelewa hivyo kuambulia kuchukua majivu ya watoto hao wawili waliaochana mwaka mmoja kuzaliwa.
Ndugu na jamaa wa karibu wakiwaaga watoto hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, SACP Onesphory Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema tofauti na madai ya baadhi ya watu kuwa baba mzazi wa watoto hao anashikiliwa na polisi, alichukuliwa na kupelekwa hospitali kwa ajili ya kutibiwa majeraha na hatachukuliwa hatua yoyote kwa vile kilichotokea ni ajali.
Aidha Kamanda Matei alitumia fursa hiyo kupiga marufuku biashara hiyo ya mafuta ya petroli na dizeli ambayo ni maarufu wilayani humo.
Wakinamama wakipanda gari kuelekea kwenye mazishi ya watoto Nuru na Dora.
Marehemu walizikwa Jumatatu iliyopita kwenye Makaburi ya Bunju, Kinondoni, Dar.
Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni