Ijumaa, 22 Agosti 2014

KUKOSEKANA WATALII KWAATHIRI MBWA NA PAKA MJINI MOMBASA KENYA


Athari za kuzorota kwa utalii katika pwani ya Kenya
Kwa miaka mingi paka na mbwa walioko chini ya shirika la kuangalia maslahi ya wanyama tawi la Mombasa, yaani Kenya Society for the Protection and Care of Animals, wamekuwa wanapata chakula kwa wingi kutoka hoteli mbali mbali mjini Mombasa pwani ya Kenya.
Mwandishi wetu John Nene anatupa tathmini kamili ya hali ilivyo.
Kila mara gari ambalo hubeba chakula chao linapowasili kwenye makao yao yalioko kaskazini mwa Mombasa kama kilomita 14 hivi kutoka katikati mwa mji huo, mbwa hao, masikio juu, hupata hamasa wakijiandaa kwa mlo mtamu wa kushibisha.
Visa vya utovu wa usalama vimewaogopesha watalii Mombasa
Paka hushiba kabisa kiasi kwamba hatimaye kazi ni kulala tu kwani kwa kawaida paka ni mnyama anayejipenda sana na mvivu pia.
Lakini sasa, kulingana na meneja wa makao hayo ya wanyama, Diana Purchase, mambo yamebadilika na hawapati tena chakula kwa wingi kama iliyokuwa kawaida yao.
Diana anatueleza ni kwa nini:"Siku hizi sisi hatupati chakula kingi kama zamani kwa sababu hakuna watalii kwenye hoteli za pwani ni wachache sana.Tunapata chakula kidogo sana na inatubidi tunanunua sisi wenyewe na hii inatulazimu tutumie pesa zaidi kwa sababu hatupati tena chakula cha bure. Hata tukipata ni kichache sana.''
Mbwa na paka wanakosa wahisani na masalio ya vyakula
Mbali na kutumia pesa za shirika hilo kununua chakula Diana anasema kuna wasamaria wema wanawasaidia na mchele kilo mia moja kwa wiki.
"Paka hupenda sana kula wali na samaki lakini mbwa wanapenda nyama zaidi, na mbwa wanakula chakula kingi kuliko paka,'' anatueleza Diana.
Ukosefu wa watalii ni kutokana na hali mbaya ya usalama mjini Mombasa na maeneo mengine ya pwani hasa kaunti ya Lamu ambayo imeshuhudia mauaji ya zaidi ya watu 100, magaidi wa kundi la Al Shabaab kutoka Somalia wakisema ni wao wamehusika na mauaji hayo.
Visa vya utovu wa usalama vimewaogopesha watalii Mombasa
Nilipotembelea paka na mbwa hao walionekana wachangamfu kiasi lakini kama wangekuwa na uwezo wa kuzungumza wangeuliza meneja Diana mbona hawapati chakula kwa wingi kama zamani.
Kuna paka wa kila aina hapo, mwingine ana miguu mitatu tu. Namuuliza Diana mbona ana miguu mitatu huyo, na anajibu:"Huyu paka aliletwa hapa akiwa hivyo, labda aliteswa sana kule alikuwa mpaka akakatwa mguu mmoja lakini yuko sawa na unaona alivyo mchangamfu.''
Mbwa na paka mjini Mombasa hufaidi mabaki ya vyakula
Hata paka weusi wapo kwenye makao hayo. Kuna baadhi ya watu wa Mombasa wanahusisha paka weusi na majini lakini Diana anakanusha akisema hizo ni fikra za ushirikina kwa miongoni mwa wakaazi wa Mombasa.
"Sisi wazungu tunapenda paka weusi kwa sababu iko na bahati sana, hawa watu wa hapa wanaamini mambo mbaya juu ya paka weusi,'' asema Diana ambaye kwake anaishi na mbwa wanne, paka tisa na ndege kasuku wawili.
Wakati mwingine watu huja kununua paka na mbwa hao. Nilishuhudia mbwa akiuzwa kwa dola 35 nilipokuwa huko. Pesa hizo, Diana anasema, zinawasaidia kwa matumini kwani mbali na chakula wanatumia pesa kutibu wanyama hao

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni