Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Peter Pinda amefungua mkutano wa Mawaziri wa Afrika wa Mazingira na Mawaziri wa Mambo ya nje kutoka katika baadhi ya nchi za Afrika jijini Dar-es-salaam leo.(Martha Magessa)
Mkutano huo ambao ufunguzi wake uliongozwa na agenda kuu iliyozungumzia mwongozo wa namna ya kushughulikia changamoto zitokanazo na athari za mabadiliko ya tabianchi, na ambavyo nchi za Afrika zitakavyoweza kunufaika na rasilimali zinazotolewa na nchi zinazoendelea ili kukabiliana na janga hilo.
Aidha Waziri mkuu Pinda alielezea kuwa mkutano huo pia una umuhimu kwa nchi za bara la Afrika pia utahusisha namna ambavyo serikali za Afrika zinaweza kukabiliana athari zitokanazo na mabadiliko ya Tabiachi. Pia alisema kuwa mkutano huu ni sehemu ya maandalizi ya mkutano mkubwa wa mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika mjini Newyork Marekani unaotegemewa kufunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Baink Moon.
"Wote tunafahamu kwamba mabadiliko ya Tabianchi yanaathari kubwa kwa dunia nzima ila madhara yake yanatofautiana kutokana na mabara, vizazi, umri, nafasi, matabaka pamoja na kipato" Aliongeza kuwa kutokana na uchumi tegemezi wa nchi nyingi za Afrika nchi hizo zimekuwa zikiathirika zaidi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kiwango kidogo cha kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya Tabianchi na kuwa na uchumi mbovu.
Aliendelea kusema kuwa Afrika na Jamii za kimataifa zinatakiwa kuwa na utashi wa kisiasa katika kuungana kwa pamoja ili kuweza kushirikiana katika kupunguza uzalishaji wa gesi joto pia katika kuhimili na kukabiliana na athari hizo.
Mkutano huo wa Mabadiliko ya tabianchi uliofanyika leo jijini Dar-es-salaam umehusisha baadhi ya Mawaziri wa Mazingira na Mawaziri wa Mambo ya nje ambao ni wajumbe wa kamati ya nchi za Afrika ya Mabadikliko ya Tabianchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni