Waziri Mkuu wa Uingereza, David
Haines.
Baada ya kundi
linalojiita 'Dola la Kiislamu' kusambaza vidio ya kukatwa kichwa kwa raia wa
Uingereza, Waziri Mkuu David Cameron ameitisha mkutano wa dharura kujadiliana
hatua za kuchukuwa.
Kikao cha Cameron na kamati maalum ya dharura
kinachofahamika kama Cobra kinafanyika baada ya vidio hiyo kuonesha David Haines
akikatwa kichwa, huku ikitishia kumuua mwengine. Wizara ya Mambo ya Nje ya
Uingereza inasema haina sababu ya kutilia shaka uhakika wa vidio hiyo.
Bado haijafahamika kile kitakachoamuliwa na kikao hicho, lakini
wachambuzi wa mambo wanasema ni wazi uamuzi utakuwa ni kulipeleka jeshi la
Uingereza moja kwa moja kwenye vita dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu.
Cobra ni kikao cha juu kabisa cha masuala ya usalama na washiriki wake
ni pamoja na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka jeshini na idara ya ujasusi,
ofisi ya mambo ya nchi za nje na wizara ya mambo ya ndani. Awali Cameron
alikilaani kitendo cha kukata kichwa kwa Haines, akikielezea kuwa "uovu mkubwa".
ACTED yalaani mauaji ya mfanyakazi wake
David Haines katika uhai wake.
Shirika la misaada ambalo
lilikuwa limemuajiri Haines, Agency for Technical Cooperation and Development
(ACTED) lenye makao yake makuu Paris, Ufaransa, limetoa tamko la kusikitishwa na
mauaji hayo na kulilaani vikali kundi la Dola ya Kiislamu.
"Mauaji ya
kutisha dhidi ya David, mfanyakazi wa misaada ya kibinaadamu, ni dhidi ya kila
msingi wa ubinaadamu, na yanaiathiri jamii nzima ya misaada ya kiutu," ilisema
taarifa hiyo huku ikiapa kuendelea kwa huduma za shirika hilo kwa wale wenye
matatizo.
Haines anakuwa raia wa tatu kutoka mataifa ya Magharibi
kukatwa kichwa ndani ya wiki chache na kundi hilo, ambalo limechukuwa udhibiti
wa eneo kubwa la Syria na Iraq, wengine wakiwa ni waandishi wa habari wa
Kimarekani, James Foley na Steven Sotloff.
Australia yatuma wanajeshi
Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott.
Katika hatua
nyengine, Australia imekuwa nchi ya kwanza kuelezea idadi ya wanajeshi na ndege
inazotuma kwenye muungano wa kupambana na wanamgambo wa 'Dola la Kiislamu'
unaoongozwa na Marekani. Waziri Mkuu Tony Abbott alisema siku ya Jumapili (14
Septemba) kwamba wanajeshi 600, ndani yake wakiwamo 400 wa angani na 200 wa
kikosi maalum watapelekwa kwenye kituo cha kijeshi cha Marekani katika Umoja wa
Falme za Kiarabu.
Abbott alisema pamoja na wanajeshi hao, Australia
itatuma ndege nane za kivita, moja ya kutoa tahadhari na udhibiti na moja ya
kujazia mafuta ndege zikiwa angani. Kwa mujibu wa waziri mkuu huyo, yote hayo
yatafanyika ndani ya siku chache zijazo.
Hata hivyo, Abbott alisema
kwamba bado hajafanya maamuzi juu kutuma wanajeshi wa moja kwa moja wa ardhini
kukabiliana na wanamgambo wa Dola ya Kiislamu, lakini haondoi uwezekano huo.
Tayari timu maalumu ya washauri wa kijeshi imeundwa kushauriana na vikosi vya
Iraq na vyombo vyengine vya usalama kwenye mapambano hayo.
Tangazo hilo
linakuja siku mbili baada ya Australia kupandisha kiwango cha kitisho cha ugaidi
katika ardhi yake, huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kwa wapiganaji wa jihadi wa
Australia wanaorejea nyumbani baada ya kupigana Syria na Iraq.
Kerry
aendelea na ziara yake Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (kushoto) na mwenzake
wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu.
Tangu Rais Barack Obama wa Marekani
kutangaza mkakati wake wa kukabiliana na kundi la "Dola la Kiislamu" katikati ya
wiki iliyopita, Waziri wake wa Mambo ya Nje, John Kerry, amekuwa kwenye ziara ya
mataifa ya Kiarabu, akisaka uungwaji mkono wa mataifa hayo kwenye operesheni
hiyo.
Tayari mataifa 10 ya Kiarabu - zikiwemo Misri, Iraq, Jordan,
Lebanon, Oman, Bahrain, Saudi Arabia na Qatar - yamekubali kujiunga na kile
kilichopewa jina la "Muungano wa Wenye Dhamira" ya kulishinda kundi hilo la
kigaidi.
Saudi Arabia kwa upande wake imetangaza kuwa tayari kuwa
mwenyeji wa kambi za mafunzo kwa waasi wa Syria wenye msimamo wa wastani
wanaopambana na kundi hilo na pia serikali ya Rais Bashar al-Assad.
Hata
hivyo, kikwazo hadi sasa kimekuwa ni Uturuki ambayo licha ya kuwa mwanachama wa
Jumuiya ya Kujihami ya NATO na jirani wa Iraq na Syria liliko kundi la Dola la
Kiislamu, imekataa kujiunga na kampeni ya kijeshi ikihofia usalama wa raia
wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni