Alhamisi, 18 Septemba 2014

MAMA WA MTOTO WA MIUJIZA AFUNGUKA

Mtoto Happiness (10) anayedaiwa kuzua kizazaa mjini Zanzibar.
MTOTO Happiness (10) (pichani) ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alizua kizazaa mjini Zanzibar baada ya kuonekana akizungumza na viumbe wa ajabu na wanyama, ametua jijini Dar kufuatia kufika kisiwani humo kimaajabu.Kwa mujibu wa mama mzazi wa mtoto huyo, Sarah Zefania, mwanaye Happiness alianza kuonesha maajabu Zenji tangu alipoonekana kwenye uwanja wa ndege kisiwani humo wiki iliyopita.
Alisema maofisa wa uwanja huo walipigwa butwaa baada ya kumwona mtoto huyo uwanjani amepita sehemu zote za ukaguzi ambazo abiria asiyekaguliwa nyaraka zake za kusafiria na mitambo maalum ya kuangalia vitu mbalimbali vikiwemo kemikali hatari, silaha na madawa ya kulevya hawezi kupita.
Kwa mujibu wa mama huyo, aliambiwa na maofisa wa uwanja huo kuwa sehemu hizo zote mtoto wake alipita bila kuonekana na kamera za uwanjani hapo wala kuacha kumbukumbu yoyote hali iliyozidi kuwaumiza vichwa maofisa wa uwanja huo.
Zefania alisema wakati maofisa hao wakitafakari hayo, ndipo msamaria mwema mmoja alijitokeza na kumchukua kwenda kumuhifadhi nyumbani kwake.Mtoto Happiness akiwa na mama yake mzazi, Sarah Zefania.
“Akiwa nyumbani kwa msamaria mwema huyo, nimeambiwa mwanangu alianza kumfanyia maajabu mbalimbali ikiwemo kuzungumza na wanyama na viumbe wengine wa ajabu au kutoka nje huku mlango umefungwa kwa ndani.
“Kuna muda alizungumza na viumbe wasioonekana ambapo aliwasiliana nao na kumletea vitu kadhaa alivyovitaka. Wakati mwingine alizungumza na wanyama wa mle ndani, kama kuku na paka ambao alikuwa akiwatuma kumfanyia yote aliyokuwa akiwaagiza.
“Hali hiyo ilimshtua yule msamaria mwema naye aliomba kupambazuke ili ampeleke mwanangu ustawi wa jamii. Yaani nahisi pengine angekuwa amemuokota sehemu bila kukabidhiwa mbele ya mashahidi pengine angemtupa usiku huohuo.
“Baada ya kushuhudia vituko hivyo, asubuhi iliyofuata alimkimbiza ustawi wa jamii ambako nako wameniambia alianza kuwafanyia vituko kama hivyo na kuwaambia kuwa angewatoroka muda wowote, kisha kuonekana akiparamia juu ya paa na kutaka kutoka.
“Yaani kwa muda mfupi waliokaa naye, maofisa wa ustawi wa jamii wanasema amewahenyesha vya kutosha ndipo walipofanya juhudi za kunitafuta na mimi nikaenda kumfuata,” alisema mama huyo muda mfupi baada ya kutua bandarini Dar.
Mtoto Happiness katika pozi.
Paparazi wetu alipomtaka mtoto huyo kuzungumza alikataa katakata na kujifanya bubu hali iliyomshangaza hata mama yake. “Nashangaa, sijui kwa nini hataki kuzungumza na wewe wakati ni mzungumzaji sana,” alisema mama Happiness.
Akizungumzia historia ya mtoto huyo, mama huyo alisema alimzalia Musoma, Mara na mwanaume mmoja aliyemtaja kwa jina la Juli ambaye walitengana na hawana mawasilino mazuri.
Mama huyo alisema alimpeleka mtoto wake shuleni lakini kila akifika harudi nyumbani na kutorokea anakokujua na kuonekana baada ya wiki mbili au tatu.
Kufuatia hali hiyo amewaomba wasamaria wema na viongozi wa dini kumwombea mtoto wake ili arudi katika hali ya kawaida kwani anajua kuna mkono wa mtu wa karibu uliyemharibu mtoto wake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni