Baraza la seneti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo
(23.01.2015) limefuta kipengele kinachotaka sensa ifanyike kabla uchaguzi
wa rais mwaka ujao katika muswada wa sheria ambao unahofiwa
utamuwezesha rais wa nchi hiyo Joseph Kabila kuendelea kubakia
madarakani wakati muhula wake sasa utakapomalizika mwaka 2016.
Baraza la seneti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limefutulia
mbali kipengele kinachotaka kufanyike zoezi la sensa kabla uchaguzi wa
rais mwaka ujao na kuidhinisha ibara ya 8 ya muswada huo uliofanyiwa
marekebisho, likisema usajili wa wapigaji kura katika daftari la wapiga
kura lazima ufanyike kwa mujibu wa muda uliowekwa katika katiba kwa
uchaguzi wa rais na bunge.Kipengele hicho, ambacho kiliidhinishwa mwishoni mwa wiki iliyopita na bunge, kimeibua maandamano ya upinzani ambapo watu wapatao 42 waliuwawa mjini Kinshasa kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, International Federation for Human Rights (FIDH).
Tume inayowajumuisha wajumbe kutoka pande zote sasa itakuwa na jukumu la kuzidurusu sehemu mbili za miswada hiyo kabla kura ya mwisho, inayotarajiwa kufanyika kabla ya kikao cha bunge kumalizika Jumatatu wiki ijayo. Zoezi la kuupigia muswada wa awali lilikuwa lifanyike jana lakini likaahirishwa hadi leo, ili kuipa nafasi tume ya baraza la seneti inayodurusu vipengele vya sheria hiyo ilikuwa bado haijakamilisha kuyachungza marekebisho yaliyopendekzewa.
"Kwa mustakabali wa nchi yetu hatuwezi kuuvuruga muswada huu. Ndio maana tunahitaji kuipa tume muda wa kukamilisha kazi yake tupate sheria itakayomridhisha kila mtu," alisema rais wa baraza la seneti Leon Kengo Wa Dondo, wakati alipowahutubia wabunge jana.
Baada ya siku tatu za maandamano utulivu ulirejea katika mji mkuu wa Kongo, Kinshasa, hapo jana, lakini machafuko yakaripotiwa katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma, mashariki mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa maafisa wa Kongo watu wanne waliuwawa katika machafuko ya Goma.
Huduma za mtandao wa mawasiliano wa intaneti ambazo zilisimamishwa wakati wa maandamano hayo zilirejeshwa kwa sehemu ndogo jana, ingawa huduma ya kutuma ujumbe mfupi bado imefungwa.
Umoja wa Mataifa waonya kuhusu machafuko
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Kongo na amezitaka pande zote husika kujizuia kufanya vurugu. Ban aidha amesema mchakato wa uchaguzi huru na wa haki sharti ufanyike kwa mujibu wa katiba ya sasa bila kucheleweshwa.
Akizungumza jana kuhusu machafuko yanayoendelea Kongo kabla kufanyika kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, kuhusu juhudi za kupambana na kundi la waasi la FDLR, naibu katibu mkuu anayehusika na tume za kulinda amani za umoja huo Herve Ladsous alisema, "Taarifa ya katibu mkuu wa Umoja wa Matiafa inaelezea wasiwasi wake kuhusu jinsi maandamano haya yalivyoshughulikiwa na vyombo vya usalama."
Ladsous pia alisema katibu mkuu alikumbusha kwamba uhuru wa kujieleza na kutoa maoni kwa waandamanaji wanaoandamana kwa amani, kwa vyombo vya habari na kila kitu kinachohusiana na uhuru wa watu kuandamana lazima uheshimiwe.
Wajumbe wa kimataifa kutoka nchi za eneo la maziwa makuu pia wamesema wameingiwa na wasiwasi kutokana na machafuko ya Kongo na wamewatolewa mwito viongozi wa nchi hiyo wafanye kila wanaloweza kuepusha machafuko zaidi na waandae uchaguzi kama inavyotakiwa katika katiba ya nchi.
Kufikia sasa jumla ya watu wapatao 42 wanaripotiwa kuuawa katika makabiliano na maafisa wa usalama, kwa mujibu wa kundi moja lililoandaa maandamano hayo. Lakini serikali, ambayo inakanusha inapania kuchelewesha uchaguzi nchini humo, kwa upande wake inasema watu 15 wamekufa, wengi wao wakiwa wevi na wahalifu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni