WATU
zaidi ya 40 wanaodhaniwa kuwa majambazi, wameteka mabasi sita ya abiria
yanayofanya safari kati ya Jiji la Arusha na Nairobi, Kenya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema atalitolea ufafanuzi leo.
Kamanda Sabas, alisema mabasi hayo
yalitekwa juzi saa 8 usiku, baada ya kufika eneo la Mbuga Nyeupe, Wilaya
ya Longido, Mkoa wa Arusha.
Taarifa zilizopatikana jijini
Arusha, zinasema baada ya majambazi hayo kuteka mabasi hayo yaliyokuwa
yakitoka Nairobi kuelekea Arusha, waliwapora mali na fedha abiria wote
waliokuwamo.
Taarifa hizo, zinasema majambazi
hayo yalifanikiwa kufanya uhalifu huo baada ya kuweka mawe barabarani,
na baada ya kuyateka mabasi hayo, waliwaamuru abiria wote kushuka na
kulala chini, huku wakipekuliwa na kutakiwa wasalimishe mali zote
walizokuwa nazo.
Dereva wa moja ya mabasi
yaliyotekwa, mali ya Kampuni ya Perfect Trans, Joseph John, aliwaambia
waandishi wa habari kuwa majambazi hayo yalikuwa na silaha za jadi
yakiwamo mapanga na mashoka.
“Kundi la majambazi lilikuwa kubwa,
yaani walikuwa kama watu arobaini hivi, wametufanyia unyama wa kutisha
kwa sababu wanawake walivuliwa nguo na vito vya thamani na wanaume
tukivuliwa viatu na kuporwa kila kitu.
“Mimi ndiye nilikuwa dereva wa
kwanza kufika na basi katika eneo hili, nilipoona mawe yamepangwa
katikati ya barabara, nilisimama ili kujua kilichokuwa kikiendelea.
“Baadaye nilipokuwa nikijaribu kuyakwepa yale mawe, nilipigwa jiwe usoni hali iliyonifanya nishindwe kuendesha gari.
“Wakati wa tukio hilo, baadhi ya
wahalifu hao walikuwa hawakufunika nyuso zao na tukio hilo lilidumu kwa
zaidi ya dakika 20, kwani kila walipokuwa wakimaliza kupekua abiria wa
basi moja, waliwaamuru warudi ndani ya basi na kuhamia katika basi
jingine,” alisema Joseph.
Dereva mwingine, Jabir Athumani wa
basi jingine la Kampuni ya Perfect, alisema baadhi ya majambazi hayo
yalikuwa yakiwataja kwa majina baadhi ya abiria na kuwaamuru watoe fedha
walizokuwa nazo.
“Kwa hiyo, tunaomba vyombo vya
ulinzi na usalama vifuatilie tukio hili kwa umakini wa hali ya juu ili
kuwanasa wahusika,” alisema Jabir.
Pamoja na hayo, alisema kuna haja
Jeshi la Polisi kurudisha ulinzi uliokuwa ukifanywa na magari ya doria
yaliyokuwa katika barabara ya Arusha–Namanga ulioondolewa Aprili, mwaka
jana.MTANZANIA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni