Ijumaa, 23 Januari 2015

MDOGO WA MFALME ABDULLA AMRITHI KAKA YAKE SAUDIA

Mfalme wa Saudi Arabia Abdullah bin Abdul-Aziz Al Saud alifariki dunia siku ya Ijumaa akiwa na umri wa miaka 90, na kurithiwa na na mdogo wake Salman, kama mtawala wa juu kabisaa wa taifa hilo tajiri wa mafuta.
Viongozi wa ulimwengu wametuma salaam za rambirambi kufuatia kifo cha Mfalme Abdullah, anaeangaliwa kama mwanamageuzi mwenye tahadhari, alieliongoza taifa hilo la kifalme katika kipindi cha misukosuko, katika kanda iliyotikiswa na joto la mageuzi katika mataifa kadhaa ya Kiarabu na itikadi kali za dini ya Kiislamu.
Ofisi ya Kifalme haikutaja sababu ya kifo cha Abdullah, lakini alilazwa hospitali mwezi Desemba akisumbuliwa na homa ya mapafu, na alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine.
Chini ya utawala wake ulioanza mwaka 2005, Saudi Arabia imekuwa mshirika muhimu wa utawala mjini Washington katika ulimwengu wa Kiarabu, ushirika wa karibuni zaidi ukiwa wa muungano wa mashambulizi dhidi ya kundi la Dola ya Kiilsamu nchini Iraq na Syria, unaoongozwa na Marekani.
Rais wa Marekani Barack Obama amemueleza Abdullah kama mshirika anaethaminiwa. Salaam nyingine za rambirambi zimetoka Japan, India, Ufilipino, Pakistana na Ufaransa na pia kutoka kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.
Mfalme mpya Salman bin Abdul-Aziz. Mfalme mpya Salman bin Abdul-Aziz.
Kifo chake chapandisha bei za mafuta
Kama taifa linaloongoza kwa uzalishaji mafuta duniani, Saudi Arabia imechangia pakubwa uamuzi wa OPEC kukataa kupunguza uzalishaji ili kusaidia bezi za mafuta, ambazo zimeshuka kwa zaidi ya asilmia 50 tangu mwezi Juni. Bei za nisahti hiyo zilipanda leo, kufuatia kifo cha Abdullah, kukiwa na wasiwasi juu y aiwapo mfalme mpya Salman bin Abdul-Aziz ataendeleza sera hiyo.
Lakini Salma amesema katika hotuba yake kwa njia ya Televisheni muda mfupi uliyopita, mflame huyo mpya mwenye umri wa miaka 79 ameahidi kuendeleza sera za watangulizi wake. "Tutaendelea kuziheshimu sera sahihi ambazo Saudi Arabia imezifuata tangu kuasisiwa kwake," alisema mfalme huyo.
Abdullah alifanya mageuzi ya tahdhari wakati akiwa madarakani, akiwapinga wahafidhina kwa hatua kama vile kuwajumlisha wanawake katika baraza la ushauri maarufu kama Shura. Aliongoza maendeleo ya kiuchumi ya falme hiyo, na alisimamia mchakato wa nchi kujiunga na shirika la biashara duniano WTO, akitumia fedha za mafuta kujenga miji mipya ya kiuchumi, vyuo vikuu na njia za reli.
Lakini Saudi Arabia bado inakosolewa kwa rekodi yake ya haki za binaadamu, ikiwemo kufungwa kwa wapinzani. Pia ndiyo nchi pekee duniani, ambako wanawake hawaruhusiwi kuendesha magari.
Mfalme Abdullah enzi za uhai wake. Mfalme Abdullah enzi za uhai wake.
Mkereketwa wa familia ya kifalme
Salman ni mkereketwa wa familia ya kifalme anayesifiwa kwa kuubadili mji wa Riyadh wakati wa kipindi cha nusu karne alichokuwa gavana wake. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na wasiwasi juu ya afya yake, baada ya kufanyiwa upasuaji mgongoni, lakini Salman alichukuwa jukumu kubwa zaidi pale matatizo ya kiafya ya Abdullah yalipomlaazimu kukaa pembeni.
Salman pia ameshikilia nyadhifa za waziri wa ulinzi na mambo ya ndani, na alikuwa sehemu muhimu ya diplomasia ya Saudi Arabia, akizitembelea mara kwa mara nchi za Magharibi. Mwaka uliyopita alifanya ziara yake ya kwanza nchini China na mataifa mengine ya Asia, katika hatua ilioonekana kama jaribio la kuelekea mashariki.
Changamoto zinazomkabili
Mfalme Abdullah alimteuwa Murqim kama naibu mrithi wa kiti cha ufalme mwezi Machi mwaka jana, katika hatua ya kihistoria iliolenga kurahisha mchakato wa urithi. Murqim, ambaye ni mkuu w azamani wa idara ya ujasusi, alikuwa mtu wa karibu sana wa Abdullah akiwa na sifa ya uliberali.
Afisa huyo wa zamani wa jeshi la anga aliezaliwa mwaka 1945, ndiye mtoto wa mwisho wa Mfalme Abdul-Aziz bin Saud, mwasisi wa taifa la Saudi Arabia. Tangu kifo cha Mfalme Abdul-Aziz mwaka 1952, kiti cha ufalme kimekuwa kikirithiwa na watoto wake. Abdul-Aziz alikuwa watoto 45 waliorekodiwa na Abdullah, Salman na Murqim walizaliwa kwa mama tofauti.
Marehemu Abdullah akiwa ndani ya Swala na baadhi ya wanafamilia ya Kifalme ya Saudi Arabia. Marehemu Abdullah akiwa ndani ya Swala na baadhi ya wanafamilia wa familia ya kifalme ya Saudi Arabia.
Mfalme mpya atakabiliwa na changamoto kubwa, hasa wakati ambapo kushuka kwa bei za mafuta kunapunguza mapato ya taifa. Saudi Arabia imeweza kuepuka machafuko yaliyoyatikisa mataifa mengi ya Kiarabu katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na matumizi makubwa ya umma.
Taifa hilo limejiwekea akiba ya fedha, lakini tayari limetabiri nakisi ya dola bilioni 38.6 mwaka huu. Wasaudia wengi walitumia mitandao ya kijamii kuomboleza kifo cha mfalme wao.
Tayari Salma amemteuwa mwanaye Mohammed bin Salman kuwa waziri wa ulinzi na mkuu wa ofisi ya Kifalme, huku mawaziri wengine wakibakia katika nyafisha zao, huku akimtangaza mjukuu wa muasisi wa taifa hilo Mohammed bin Nayef kuwa naibu mrithi wa kiti cha ufalme.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni