Khadija
Ahmad, mke wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh
Ponda Issa akiondoka katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Morogoro jana baada ya kesi inayomkabili mumewe kuahirishwa hadi
Februari mwaka huu. Picha na Juma Mtanda.
Na Hamida Shariff, Morogoro.
Shahidi wa pili katika kesi inayomkabili Kiongozi wa Taasisi na Jumuiya
za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda ameieleza Mahakama ya
Hakimu Mkazi, Morogoro kuwa, hawakuhusika kumpiga risasi mtuhumiwa huyo
na kwamba alikamatwa katika Hospitali ya Muhimbili akitibiwa jeraha
alilodai lilitokana na risasi.
Akitoa
ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo shahidi Jafert
Kibona, ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
Morogoro, alisema Agosti 9, 2013, polisi walipata taarifa kuwa, Sheikh
Ponda angekwenda Morogoro kwenye kongamano, hivyo waliwataka waandaaji
kumsalimisha polisi kiongozi huyo.
Kibona ambaye kwa sasa ni
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mtwara, alisema polisi walimtaka
Sheikh Ponda kujisalimisha kutokana na kutafutwa kwa tuhuma za kutoa
maneno ya kashfa na uchochezi, Dar es Salaam na Zanzibar.
Hata
hivyo, Sheikh Ponda alikaidi amri hiyo, badala yake aliendelea kutoa
maneno ya kashfa na uchochezi katika kongamano la Morogoro, alidai
shahidi huyo mahakamani hapo.
Alidai walishindwa kumkamata
Ponda baada ya wafuasi wake kumwingiza kwenye gari dogo na kumtorosha,
kabla ya kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuwa kiongozi huyo
alijeruhiwa kwa risasi bega la mkono wa kulia.
Kibona
alisema walikwenda Hospitali Mkoa wa Morogoro, lakini hawakumkuta Ponda
na siku iliyofuata walipata taarifa kuwa amelazwa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili. Wakili wa utetezi, Juma Nassoro alimuuliza shahidi huyo
kuhusu mtu aliyempiga risasi Ponda, ikiwa polisi ndiyo pekee waliokuwa
na silaha siku hiyo.
Aliuliza pia kwa nini polisi walishindwa kumkamata Ponda wakati hakuwa na silaha. Kesi itatajwa tena Februari 2 na 19 mwaka huu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni