Mkuu wa ujumbe wa waangalizi Umoja wa Ulaya nchini Nigeria amesema
hawatawapeleka maafisa wao katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa
hilo kutokana na kitisho cha mashambulizi ya Boko Haram
Uamuzi huo wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya ambao
tayari ulituma kundi la maafisa tangu mwezi Novemba mwaka jana kwenda
Nigeria umeelezea wasiwasi kuwa ukosefu wa usalama kaskazini mashariki
mwa Ngeria huenda ukaathiri uchaguzi mkuu.Ujumbe huo umesema ikizingatiwa uadilifu unaoambatana na zoezi la uangalizi wa uchaguzi, ukosefu wa usalama kutokana na uasi huenda ukawa na athari kubwa dhidi ya demokrasia ya nchi hiyo. Mkuu wa ujumbe huo wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya nchini Nigeria Santiago Fisas amesema ni vigumu kwao kutuma waagalizi wao.
Vyombo vya habari vitafuatiliwa
Kwa mara ya kwanza katika shughuli zao za uangalizi wa chaguzi nchini Nigeria, Umoja wa Ulaya unapanga kuanzisha mpango wa kuvifuatilia vyombo vya habari nchini humo ili kuhakikisha kuwa ripoti zao kuhusu chaguzi haziegemei upande mmoja.
Hannah Roberts ambaye ni naibu wa mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa umoja wa Ulaya amesema vyombo vya habari 14 vya redio,televisheni na mageti ya kibinafsi na serikali yatafuatiliwa kuhakikisha kuna usawa katika kuviangazia vyama vyote vya kisiasa.
Licha ya kuwa ujumbe huo wa waangalizi wa umoja wa Ulaya umesema vyama vya kisiasa nchini Nigeria viliendesha teuzi zao kwa muda uliotarajiwa, unabashiri kuna hatari ya demokrasia kuathirika kutokana na mfumo wa vyama vikuu vimedhibiti ni nani anaweza kugombea na hakuna uwezekano wa kuwania kama mgombea huru,s heria ina kanuni chache kushughulikia hilo na tume ya uchaguzi haina mamlaka ya utekelezaji.
Mapendekezo ya umoja wa Ulaya hayakuzingatiwa
Umoja wa Ulaya umesema kati ya mapendekezo hamsini iliyowasilisha kwa serikali ya Nigeria baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2011, ni pendekezo moja tu lililotekelezwa kufikia sasa ambalo ni sheria kuhusu uhuru wa kutolewa taarifa na hivyo ina wasiwasi kuwa matatizo yaliyohusishwa na uchaguzi huo uliopita bado yatakuwepo kipindi hiki.
Hayo yanakuja huku tume ya uchaguzi nchini Nigeria ikisema itaendelea mbele na mpango wa kuendesha uchaguzi kama ilivyopangwa kwenye ratiba ya uchaguzi na kupuuzilia mbali wito kutoka kwa mmoja wa washauri wa Rais kuwa chaguzi ziahirishwe.
Mpaka sasa wapiga kura takriban milioni 30 hawajapata kadi za kupigia kura kuweza kushiriki katika uchaguzi wa kwanza Nigeria wa kutumia kadi za kura za kieletroniki hatua ambayo inatarajiwa kuzuia udanganyifu kama ulioshuhudiwa katika chaguzi zilizopita. Kiasi ya wapiga kura milioni 68.8 wanatarajiwa kushiriki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni