Rais Barack Obama alitumia hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa kuwaonya
wajumbe wa Congress kutothubutu kuyazuia mageuzi ya kisiasa na kiuchumi
katika hotuba inayoitwa kuwa cha uthubutu wa urais.
Ni hotuba ya kwanza ya Rais Obama kwenye Congress tangu wapinzani wake
wa Republican kuchukuwa udhibiti wa mabaraza yote mawili ya kutunga
sheria nchini Marekani, na bila ya shaka ulikuwa uwanja wa mapambano ya
kisiasa, ambao alipigana vyema, akitetea sera zake za ndani na nje,
katika hotuba iliyoangaliwa na mamilioni ya watu kupitia televisheni
zao.Akitangaza rasmi kumalizika kwa mkwamo wa kiuchumi ambao utawala wake uliurithi na kupambana nao kwa miaka sita mutawaliya, Rais Obama ameitaka Congress kuyatunza mafanikio hayo kwa kuwapandishia kodi matajiri na kutokuzivuruga sera za huduma ya afya na uhamiaji.
"Kwa hivyo, uamuzi wa hukumu uko wazi. Uchumi wa tabaka la kati unafanya kazi, ikiwa tu siasa zetu hazitaukwamisha. Hatuwezi kuhatarisha usalama wa familia kwa kuwanyang'anya bima zao za afya au kuweka kanuni mpya kwenye Wall Street au kupigana tena vita vya kale juu ya uhamiaji, katika wakati ambapo tunapaswa kuunda mfumo uliobomoka. Na kama kutakuja mswaada wowote wa sheria mezani kwangu kufanya chochote kati ya hayo, nitaupigia kura ya turufu," alisema Obama.
Obama anataka sehemu kubwa ya fedha za kodi iliyopandishwa kwa matajiri zitumike kuinua tabaka la kati, akihoji kwamba Marekani haiwezi kuendelea ikiwa uchumi wake unawanufaisha wachache na kuwaacha wengi wakiwa masikini.
Republican wajibu
Tayari chama cha Republican kimeijibu hotuba hiyo kwa kusema kwamba Rais Obama anatumia njia ile ile iliyoshindwa kutatua matatizo yale yale siku zilizopita. Akiwasilisha jibu hilo la Republican, Seneta Joni Ernest alisema sera ya huduma ya afya ya Rais Obama, maarufu kama Obamacare, haijibu matatizo yaliyomo kwenye mfumo wa afya.
"Wamarekani wamekuwa wakiumizwa, lakini kila tulipodai suluhisho, mara zote serikali ilijibu kwa akili ile ile finyu ambayo ilipekelea sera zilizoshindwa kama ile ya Obamacare. Ni akili ambayo inatupa jukwaa la kuzungumza kisiasa, lakini sio suluhisho la kweli," alisema seneti huyo mpya.
Kuhusiana na sera zake za nje, Obama alitetea uamuzi wake wa hivi karibuni wa kurekebisha mahusiano kati ya nchi yake na Cuba na kuitaka Congress iidhinishe fedha zaidi kwa ajili ya kampeni ya kijeshi dhidi ya kundi lijiitalo Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria, akiapa kwamba chini ya miaka miwili iliyobakia ya utawala wake, Marekani itaendelea kupambana na ugaidi ulimwenguni kote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni