Jumatano, 25 Februari 2015

CHENGE AKATAA KUHOJIWA NA BARAZA LA MAADILI KTK SAKATA LA ESCROW

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) Andrew Chenge akitoka katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo.
...Akihojiwa na wanahabari waliokuwepo eneo la tukio.

...Akipanda gari lake kuondoka katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo.
ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) Andrew Chenge amekataa kuhojiwa mbele ya Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma juu ya tuhuma za kunufaika na fedha zilizotoka katika akaunti ya Tegeta Escrow, wakati alipoitika wito katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo.
Chenge alitajwa kuwa mmoja wa watu waliopewa fedha na Mkurugenzi wa kampuni ya PAP, James Rugemalila, zilizotolewa katika akaunti hiyo ya umma ambayo ilikuwa ikihifadhi hela za Tanesco na IPTL, kiasi cha shilingi bilioni 1.6, kitendo kilichosababisha kuondolewa katika nafasi ya Uenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini baada ya kufika mbele ya kikao cha Baraza hilo, kilichokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, Chenge alisema hawezi kuhojiwa na kikao hicho kwa vile suala lake tayari lipo mahakamani, kauli iliyomfanya Jaji (mst) Msumi na wajumbe Selina Wambura na Hilda Gondwe kukosa la kufanya.
Baadaye Jaji Msumi aliwaambia waandishi wa habari kuwa atatoa tamko la Baraza kuhusu suala hilo kesho, huku likijiandaa pia kuwaita na kuwahoji wanasiasa wengine, akiwemo Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye naye alipewa kiasi kama hicho cha fedha.
Wengine watakaoitwa kuhojiwa ni pamoja na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mkuu wa wilaya ya Korogwe, Mrisho Gumbo na kiongozi mwandamizi wa Ikulu, anayetajwa kwa jina la Shaaban Gurumo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni