Jumamosi, 14 Februari 2015

MAPAMBANO MAKALI UKRAINE

Mapigano makali yaendelea Ukraine Jumamosi (14.02.2015) na kutishia makubaliano ya kusitisha mapigano wakati serikali na Marekani zikiishutumu Urusi kwa kuchochea mashambulio ya waasi kuteka ardhi zaidi kabla ya suluhu.
Mwanajeshi wa Ukraine. Mwanajeshi wa Ukraine.
Mkuu wa polisi wa mji mkuu wa Kiev Vyacheslav Abroskin amesema mashambulizi ya mizinga bila ya kusita yamekuwa yakiutekeza mji wa Debalitseve ambacho ni kituo kikuu cha usafiri wa reli kinachoshikiliwa na vikosi vya serikali.
Abroskin ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook mtandaoni kwamba waasi wanauangamiza mji wa Debaltseve ambapo maeneo ya makaazi ya watu na majengo yamekuwa yakishambuliwa bila ya kusita na mizinga.

Kikosi cha wapiganaji wa kujitolea cha Azov pia kimeripoti kuwepo kwa mapigano makali mashariki mwa mji muhimu unaoshikiliwa na serikali wa Mariupol na kwamba kijiji cha Shyrokyne kimeharibiwa kabisa na mashambulizi ya mabomu.
Makubaliano ya amani hatarini
Rais Petro Poroshenko. Rais Petro Poroshenko.
Rais Petro Poroshenko wa Ukraine ameonya hapo Ijumaa kwamba kupamba moto kwa mapigano kumeyatumbukiza makubaliano yaliofikiwa katika mji wa Belarus Minsk baada ya mazungumzo ya muda mrefu na Rais Vladimir Putin wa Urusi katika hatari kubwa kabla ya hata kuanza kutekelezwa.
Akizungumza kwa lugha ya Kingereza Poroshenko amesema baada ya makubaliano hayo ya Minsk operesheni ya Urusi imepamba moto sana.
Usitishaji huo wa mapigano unatazamiwa kuanza saa sita usiku Jumamosi utakuwa mtihani wa kwanza wa kujitolea kwa serikali ya Ukraine na waasi wanaoegemea upande wa Urusi kwa makubaliano hayo mapya ya amani yaliosainiwa Alhamisi.
Lakini wakati serikali ya Ukraine na Marekani zikidai kwamba Urusi ilikuwa inaongoza mashambulizi hayo ya waasi ya kuteka ardhi zaidi huku vikosi vya serikali vikijichimbia kuyahami maeneo hayo,kuna hofi hofu iwapo suluhu hiyo itazingatiwa.
Poroshenko usiku huu anatazamiwa kuzungumza na Rais Barack Obama wa Marekani,Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitarajiwa kukutana Jumapili kwa kikao cha dharura.
Makubaliano yasiokuwa na mwamko
Kifaru cha kikosi cha serikali ya Ukraine. Kifaru cha kikosi cha serikali ya Ukraine.
Marekani imesema jeshi la Urusi limeweka idadi kubwa ya mizinga na zana za kuvurumishia maroketi ambapo wanatumia kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na vikosi vya serikali.
Msemaji wa usalama wa Ukraine Andriy Lysenko amesema kwamba waasi wakisaidiwa na jeshi la kawaida la Urusi wamekuwa wakijaribu kufanikisha malengo muhimu ya kimkakati kutanuwa eneo la ardhi wanayoishikilia kabla ya kuanza kwa usitĂ­shaji huo wa mapigano.
Lysenko amesema wanajeshi saba wameuwawa na 23 kujeruhiwa katika mapigano ya kipindi cha saa 24 zilizopita wakati waasi na maafisa wa serikali wanasema raia watatu wameuwawa.
Serikali ya Ukraine na mataifa ya magharibi yamekuwa yakiishutumu Urusi kwa kupeleka silaha na wanajeshi nchini Ukraine kuwasaidia waasi.Ikulu ya Urusi imekuwa ikikanusha mara zote madai hayo lakini waasi hao wanaoegemea upande wa Urusi wamekuwa wakijivunia silaha za kisasa zinazotumiwa na majeshi ya kawaida na mara nyingi wamekuwa wakivizidi nguvu vikosi vya Ukraine.
Marekani kutuma silaha Ukraine
Waasi mashariki mwa Ukraine Waasi mashariki mwa Ukraine.
Obama ameonya kwamba ataanza kupeleka silaha Ukraine iwapo makubaliano hayo ya mapya ya amani yatasambaratika.
Ngurumo za mashambulizi mazito ya mizinga pia zimekuwa zikisikika kwenye mji ulio ngome kuu ya serikali wa Donetsk.
Merkel ameionya Urusi kwamba Umoja wa Ulaya ambayo umeiwekea Urusi vikwazo kadhaa kutokana na mzozo huo haiondowi uwezekano wa kuchukuwa hatua zaidi iwapo makubaliano hayo ya suluhu yatashindwa.
Kundi la G7 laonya
Viongozi wa nchi wanachama wa kundi la G7. Viongozi wa nchi wanachama wa kundi la G7.
Mataifa ya Kundi la Mataifa Saba yenye Maendeleo Makubwa ya Viwanda Duniani G7 ya Canada, Ufaransa,Ujerumani,Italia, Japani, Uingereza na Marekani pia yameelezea wasi wasi wao juu ya umwagaji damu huo na kulimbikizwa kwa silaha mashariki ya Ukraine.
Kundi hilo limeonya kwamba liko tayari kuchukuwa hatua kali kwa yoyote yule atakayekiuka masharti ya makubaliano hayo.
Makubaliano hayo tete yalikuwa yakionekana kama matumaini mazuri ya kukomesha mzozo huo ambao umeuwa watu 5,480 na kuuweka mvutano kati ya mataifa ya mashariki na magharibi katika hali mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea kumalizika kwa Vita Baridi lakini mashaka yameendelea kuwepo baada ya kusambaratika kwa mpango wa makubaliano ya amani kama huo uliopita.
Viongozi wa waasi ambao mataifa ya magharibi wanawaona kuwa ni vibaraka wa Urusi wamesema makubaliano hayo mapya yanaleta matumani ya amani lakini wameonya kwamba hakutokuwa na mazungumzo zaidi iwapo makubaliano haya ya sasa yatashindwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni