Shirika la haki za binaadamu Human Rights Watch limesema katika ripoti
yake mpya kuhusu Burundi, kwamba majeshi ya nchi hiyo na polisi
walifanya mauaji ya watu takriban 47 kati ya Desemba 30 2014 na Januari 3 mwaka
huu 2015.
Mauwaji hayo yalifuatia mapigano yaliozuka dhidi ya kundi la watu
waliokuwa na silaha katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Cibitoke
(CHIBITOKE). Ripoti ya Shirika hilo imesema vijana wa chama tawala
waliokuwa na silaha pia walishiriki katika mauaji hayo.Mkurugenzi wa Shirika hilo anayehusika na Afrika Daniel Bekele amesema majeshi ya Burundi yana wajibu wa kuwalinda raia dhidi ya machafuko na matumizi ya nguvu, lakini haina maana kuwauwa wale iliowakamata. Akaongeza kwamba inaelekea wanajeshi na Polisi hawakufanya jitihada yoyote kuwakamata watu waliosalimu amri, lakini badala yake wakawapiga risasi.
Mauaji ya Cibitoke ni sehemu ya mpango mpana wa mauaji wa majeshi ya Burundi na wanachama wa Umoja wa vijana wa chama tawala CNDD-FDD wnaojulikana kama Imbonerakure, matukio yanayoanzia miaka mingi nyuma. wahanga wa mauaji hayo ni pamoja na raia na wanachama wa makundi yenye silaha pamoja na wale wanaotuhumiwa kuwa wapinzani. Mauaji ya Cibitoke ni moja wapo ya matukio makubwa kabisa ya aina yake katika miaka ya karibuni .
Taarifa chache zilizopatikana kuhusu kundi moja lililokuwa na silaha , zinaeleza kwamba lilivuka mpaka kuingia Burundi kutokea nchi jirani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mwezi Desemba mwaka jana. Mashahidi na duru za kijeshi zinasema waliohusika walikuwa wamejizatiti kwa silaha. baadhi ya waliokamatwa waliliambia Shirika la Human Rights watch kwamba lengo lao lilikuwa kuunda kambi msituni mashariki mwa Cibitoke, ambako zingetokea harakati zao dhidi ya serikali ya Burundi.
Mashahidi wamesimulia mauaji mwanzoni mwa mwezi Januari, katika msitu wa Kindindi karibu na wilaya za Mpinga na Murwi na pia baina ya milima ya Ngoma na Rugano, wakishiriki pia vijana wa Imbonerakure neno lenye maana ya " Muuwe huyo mbwa."
Mkurugenzi wa Afrika wa Shirika la haki za binadamu human Rights watch Bekele, amesema maafisa wa Burundi wanapaswa kufanya uchunguzi ulio wazi na kuhakikisha wahusika wamefikishwa mbele ya sheria. Mara nyingi tume zilizopita kuhusiana na uchunguzi wa matukio ya aina hiyo zilichukua msimamo wa kisiasa. Ripoti hiyo ya Human Rights watch inaelezea matukio mengi .
Wizara wa mambo ya nchi za nje ya Marekani ilisema katika taarifa tarehe tano mwezi huu, kwamba inasumbuliwa na ripoti ya kuhusika majeshi ya usalama ya Burundi katika mauaji ya wanachama 24 wa kundi moja la waasi baada ya kujisalimisha mapema mwezi uliopita mkoani Cibitoke.
Human Rights watch limesema nchi kama Uholanzi zinaisaidia Polisi ya Burundi na Marekani inalipa msaada jeshi la Burundi. Limezitaka nchi hizo zishinikize pafanyike uchunguzi huru na wa uwazi na kuifahamisha wazi serikali ya Burundi kwamba hawatoweza kuendelea kuzisaidia taasisi au vikosi vinavohusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, na kwamba maafisa wanajukumu la kuwawajibisha wahusika kwa kuwafikisha mahakamani
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni