Jumatatu, 23 Februari 2015

OBASANJ AJIONDOA KWENYE CHAMA TAWALA

Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo amejiondoa katika chama tawala cha People's Democratic Party PDP hatua ambayo ni pigo kwa Rais wa sasa Goodluck Jonathan anayegombea muhula mwingine madarakani
Obasanjo ambaye ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za kikanda na ambaye ni mlezi wa kisiasa wa wanasiasa wengi nchini Nigeria, ameelezea kwa muda sasa kuvunjwa moyo na uwezo wa Rais Jonathan katika kushughulikia kitisho cha kundi la waasi la Boko Haram na kupambana na kashfa za ufisadi katika sekta ya mafuta.
Katika taarifa aliyoitoa hii leo, Rais huyo wa zamani wa Nigeria amesema kuanzia sasa atakuwa raia wa kawaida wa Nigeria na yuko tayari kushirikiana na yeyote bila ya kuzingatia misingi yake ya kisiasa.
Bila Nigeria hakuna PDP
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa Obasanjo mwenye umri wa miaka 77 aliichana kadi yake ya uanachama wa PDP nyumbani kwake hapo jana na kusema bila ya Nigeria hakuwezi kuwa na PDP na kwa hivi sasa kile anachokizingatia yeye na ni kuifanya Nigeria kuwa imara.
Rais wa sasa wa Nigeria Goodluck Jonathan Rais wa sasa wa Nigeria Goodluck Jonathan
Msemaji wa chama cha PDP Olisa Metuh amesema chama hicho kimesitikitishwa mno kuwa Obasanjo ambaye alipewa fursa ya kuliongoza taifa la Nigeria kwa miaka minane kupitia chama tawala amechukua uamuzi wa kujiondoa chamani wakati muhimu kama huu.
Kujiondoa kwa Obasanjo kutoka chama hicho ambacho alikisaidia kukua katika kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini Nigeria baada ya kutawala kama kiongozi wa kijeshi miaka ya sabini na kuhudumu kwa mihula miwili katika utawala wa kiraia kuanzia mwaka 1999 sio jambo la kushangaza.
Katika mahojiano na jarida la Finacial Times wiki iliyopita, Obasanjo aliashiria kumuidhinisha mpinzani wa Jonathan Muhammadu Buhari wa chama cha upinzani cha All Progressive Confgerss APC ambaye alikuwa kiongozi wakati wa utawala wa kijeshi katika miaka ya themanini na aliyeonekana kuwa na msimamo thabiti kuhusu masuala ya usalama na ufisadi.
Obasanjo hajaridhishwa na Jonathan
Mwaka 2013, Obasanjo alimuandikia Jonathan barua akimhimiza asigombee muhula wa pili, akiufananisha utawala wake na ule wa Jenerali Sani Abacha ambaye wakati wa utawala wake wa miaka mitano katika miaka ya tisini, kulikuwa na visa vya ukiukaji wa haki za binadamu na uporaji wa mali ya umma.
Mgombea urais wa chama ca upinzani cha APC Muhammadu Buhari Mgombea urais wa chama ca upinzani cha APC Muhammadu Buhari
Obasanjo pia ametilia shaka uongozi wa Jonathan katika kitabu cha wasifu wake kilichozinduliwa mwezi huu ambacho kimepigwa marufuku nchini Nigeria. Jeshi la Nigeria limemshutumu Obasanjo kwa kuingiza siasa katika masuala ya usalama wa taifa na masuala ya kijeshi.
Uchaguzi wa rais wa Nigeria ulikuwa ufanyike Jumamosi iliyopita lakini uliahirishwa kwa wiki sita kwa sababu za kiusalama. Tarehe mpya ya uchaguzi huo ni tarehe 28 mwezi Machi. Na iwapo kujiondoa kwa Obasanjo kutoka PDP kutakuwa na athari yoyote katika kumrudisha tena madarakani Jonathan ni jambo la kusubiriwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni