Picha: Jeshi la Kujenga Taifa likionesha ukakamavu wao hivi karibuni - Maktaba.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
JESHI
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia vijana watano
wa kundi la wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa tuhuma za
kufanya uchochezi na kufanya mikusanyiko isiyo halali jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza na
waandishi wa habari, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema vijana hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti kwa
makosa ya kuunda kikundi kisicho halali kwa mujibu wa sheria za nchi na
kuwahamasisha wenzao, kuandamana hadi Ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete
kudai ajira za kudumu.
“Tunawashikilia vijana watano ambao ndio
viongozi wa kikundi kinachojiita umoja wa wahitimu wa Jeshi la Kujenga
Taifa. Mwenyekiti ndio alikuwa wa kwanza kukamatwa na wengine
tuliwakamata juzi mara baada ya kukusanyika eneo la Msimbazi Centre na
Muhimbili,” alisema Kova.
Akieleza chanzo cha vijana hao kutaka
kuandamana kuelekea Ikulu, alidai wahitimu hao wanadai kuahidiwa ajira
za kudumu walipomaliza mafunzo yao na hivyo baada ya kukaa kwa muda
mrefu bila kuajiriwa, ndipo wakaamua kuanzisha kikundi hicho ili kwenda
kumwona Rais Kikwete kumweleza tatizo la ajira linalowakabili.
“Vijana
hawa wanadai kuwa waliahidiwa kupewa ajira za kudumu mara baada ya
kumaliza mafunzo yao ya JKT. Jambo hili sio la kweli, kwani tumefanya
uchunguzi na kubaini hakuna mkataba wowote unaosema wakimaliza mafunzo
lazima waajiriwe, bali kila mtu anatakiwa kutumia ujuzi alioupata
kujiajiri. Lakini walipokaa kwa muda mrefu bila kuona ahadi yao
inatekelezwa, wakaamua kuanzisha kikundi chao ambacho sio halali kwa
mujibu wa sheria za nchi. Hadi sasa tumeandaa jalada la mashitaka na
tumelikabidhi kwa mwanasheria wa serikali kwa ajili ya kuwafikisha
mahakamani watuhumiwa hawa kujibu mashitaka yanayowakabili,” aliongeza
Kova katika taarifa yake.
Alitaja vijana wanaoshikiliwa na
Polisi kuwa ni Mwenyekiti wa kikundi hicho George Mgoba (28) mkazi wa
Mabibo Loyola, Katibu wao Linus Emmanuel (28) mkazi wa Tabata, Emmanuel
Richard (28) mkazi wa Kawe, Jacob Joseph (36) mkazi wa Mabibo na Rizione
Ngowi (27) mkazi wa Mtoni Mtongani.
Akizungumzia tuhuma za
kutekwa na kuteswa kwa George Mgoba, Kova alisema Jeshi la Polisi
linaendelea na uchunguzi ili kubaini tukio hilo kama ni la kweli na
kwanini watu hao walimteka.
“Tunaendelea na uchunguzi kubaini
kama ni kweli kijana huyo alitekwa kama anavyodai kuwa Februari 16
alitekwa na kupatikana tarehe 19 majira ya saa nne usiku huko Tungi
Kibaha kandokando ya barabara, pia tujue ni akina nani walimteka na
kwasababu zipi kisha watu hao tutawapeleka mahakamani,” alisema Kova.
Kova
alieleza kuwa “Februari 22 mwaka huu majira ya saa kumi na moja jioni,
George Mgoba alijaribu kutoroka wadini katika Hospitali ya Muhimbili
lakini polisi walibaini ujanja wake na kufanikiwa kumweka kizuizini.
Lengo lake ilikuwa ni kukimbia matibabu na kuzua hofu kwa wananchi”.
Kwa sasa Mwenyekiti huyo wa vijana hao, bado amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akipatiwa matibabu.
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja katika
Hospitali hiyo ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa hali ya
mtu huyo, inaendelea vizuri na afya yake imeimarika.
Wakati huo
huo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari baadaye jana, Kova
alimtaka Makamu Mwenyekiti wa Vijana hao, Parali Kiwango (25) mkazi wa
Temeke Mikoroshini ajisalimishe mara moja Polisi kwa ajili ya mahojiano
zaidi, kabla jeshi hilo halijaanza kumtafuta.
“Jeshi la Polisi
linamtaka Makamu Mwenyekiti ajisalimishe mara moja kwani jana alipoona
Katibu wake amekamatwa alikimbia na kutokomea kusikojulikana. Yeye kama
ni mhitimu wa JKT hatakiwi kukimbia, bali ajisalimishe mwenyewe katika
ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam au kituo
chochote cha Polisi kilicho karibu na alipo,” aliongeza Kova.
HABARILEO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni