Alhamisi, 5 Machi 2015

WATANO WAUAWA KWA KUTUHUMIWA KUZUIA MVUA MKOANI MARA

Jeshi la polisi mkoa wa Mara limewakamata watu saba wakiwemo viongozi wawili wa Serikali ya kijiji cha Park Nyigoti katika kata ya Ikoma wilayani Serengeti mkoani Mara baada ya kutuhumiwa kuwakamata na kuwafunga vitambaa usoni watu wanane wanaowatuhumu kwa uchawi kisha kuwachapa viboko na kusababisha vifo vya watu watano. 
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Kamishina msaidizi wa jeshi la polisi ACP Ernest Kimola, amesema katika tukio hilo limesababisha watu wengine watatu kujeruhiwa na viboko hivyo na kulazwa katika hospitali teule ya Nyerere DDH Mjini Mugumu wilayani Serengeti.
Amesema mbali na mwenyekiti na mtendaji wa serikali ya kijiji kukamatwa pia viongozi wawili wa jadi wamekamatwa wakihusishwa na mauaji hayo.
Amesema kabla ya kuwakamata wananchi hao wakiwa katika miji yao kisha kuwafunga vitambaa usoni na kuwachapa viboko hadi kufa kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya ushirikina, viongozi hao wa jadi kwa kushirikiana na Serikali ya kijiji waliitisha mkutano kwa lengo la kuwabaini watu wanaojihusisha na ushirikina ambao umesababisha mvua kutonyesha kijijini hapo ambapo watu wanane walitajwa katika mkutano huo.
Kaimu kamanda huyo wa polisi mkoa wa Mara, amewataja waliouawa katika tukio hilo lililotokea alfajiri ya tarehe 2.3.2015 kisha miili yao kutupwa karibu na miji yao kuwa ni Nyahita Nyambeho, Nyasari Holela, Joseph Msoba, Nyangi Nyakitambara na Nyangi Kanyaro wote wakazi wa kijiji hicho ambapo Raphael Holela, Masenze Nyamsero na Elizabeth Mwita wamelazwa katika hospitali ya Nyerere DDH baada ya kuchapwa viboko na kujeruhiwa vibaya.
Hadi sasa jeshi la polisi mkoa wa Mara kwa kushirikiana na polisi wilayani Serengeti wanaendesha operesheni kali katika kuwasaka watu wote waliohusika kufanya mauaji hayo ya kinyama.
Vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi vimeendelea kulaaniwa kwa kuwa ni kinyume cha sheria. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni