Jumapili, 5 Aprili 2015

Al- Shabab yaonya kufanya mashambulizi zaidi Kenya

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu wa itikadi kali al-Shabab limeonya kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya Kenya kama lile walilofanya Chuo Kikuu cha Garissa lililouwa watu 148.
Kundi la wanamgambo wa Somalia la al -Shabab. Kundi la wanamgambo wa Somalia la al -Shabab.
Kwa mujibu wa shirika la uchunguzi wa kijasusi CITE, taarifa iliyotumwa na kundi hilo kupitia mtandao wao siku ya Jumamosi (Aprili 4) imesema "miji ya Kenya itachuruzika michirizi ya damu."
Wanamgambo hao wa itikadi kali za Kiislamu wamesema shambulio la chuo cha Garissa ni kulipiza kisasi kwa mauaji yaliofanywa na vikosi vya Kenya wakati wakipamnana na waasi wa kundi hilo nchini Somalia.
Taarifa yao iliotolewa kwenye tovuti zenye mafungamano na al-Shabaab na mitandao ya Twitter imesema hivyo vitakuwa vita virefu vya ukatili ambapo raia ndio watakaokuwa wa kwanza kukabiliana na maafa.
Taarifa hiyo ya al-Shabaab imesema hakuna hatua zozote zile za tahadhari au usalama zitakazoweza kuwahakikishia usalama wao,kuzima shambulio jengibe au kuzuwiya umwagaji damu mwengine.

Shambulio la al-Shabab kujibiwa
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya Jumamosi amewaonya wapiganaji wa al-Shabab kwamba serikali yake itajibu kwa hatua kali kabisa shambulio lao lililouwa takriban wanafunzi 150.
Akizungumza katika hotuba ya taifa kwa njia ya televisheni kutoka mji mkuu wa Nairobi na kutangaza siku tatu za maombolezo ya taifa amesema "Siku ya Alhamisi ilijeruhi Kenya,Alhamisi ilizijeruhi familia,marafiki na jamii za wahanga wa shambulio hilo.
Amesema kundi hilo la al-Shabab halitoweza kuunda taifa la Kiislamu ndani ya Kenya na kwamba nchi yake itafanya kila iwezalo kulinda mfumo wao wa maisha na ameomba msaada zaidi kutoka kwa jamii ya Waislamu nchini humo kutokomeza watu wenye itikadi kali.
Kenyata amesema vita dhidi ya ugaidi vimezidi kuwa vigumu kutokana na ukweli kwamba watu wanaopanga na kugharamia unyama huo wamejichimbia ndani ya jamii.
Watu watano mbaroni
Vikosi vya usalama vya Kenya nje ya Chuo Kikuu cha Garissa. Vikosi vya usalama vya Kenya nje ya Chuo Kikuu cha Garissa.
Afisa wa serikali nchini Kenya amekaririwa akisema watu watano wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika katika shambulio la Garissa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani nchini Kenya, Mwenda Njoka, amesema kwenye mtandao wa Twitter kwamba mashirika ya ujasusi nchini Kenya yamewakamata watu watatu waliokuwa wakijaribu kuvuka mpaka na kuingia Somalia. Amesema watu hao watatu ni washirika wa Mohamed Mohamud ambaye pia anajulikana kwa jina la Dulyadin Gamadhene mwalimu wa zamani wa chuo cha Madrasa ya Kiislamu nchini Kenya ambapo serikali inasema aliratibu mashambulio hayo ya Garissa.
Serikali ya Kenya imetowa bakshishi ya dola 220,000 kwa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwake.Watuhumiwa wengine wawili walikamatwa katika chuo cha Garissa mmoja akiwa mlinzi wa chuo na wa pili ni Mtanzania aliyetambulika kwa jina la Rashid Charles Mberesero.
Wanafunzi wakiondolewa nje ya Chuo Kikuu cha Garissa Wanafunzi wakiondolewa nje ya Chuo Kikuu cha Garissa.
Mtu aliyenusurika mauaji ya Chuo Kikuu cha Garissa amepatikana Jumamosi ikiwa ni siku mbili baada ya mashambulizi ya wanamgambo wa itikadi kali yaliouwa watu 148.
Cynthia Cheroitich mwenye umri wa miaka 19 ameliambia shirika la habari la AP kwamba alikuwa amejificha ndani ya kabati na kujifunika nguo na aligoma kutoka hata pale wasichana wengine walipotoka baada ya kuamuriwa kufanya hivyo na wanamgambo hao. Kwa mujibu wa polisi ya Kenya aliokolewa kabla ya saa nne asubuhi.
Maafisa wa serikali waliionyesha miili ya wanamgambo wanne wanaodaiwa kuhusika na mashambulizi hayo kwa umati wa watu 2,000 kwenye eneo la wazi katikati ya Garissa wakiwa kwenye gari ya "pick-up" lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo wa pole.
Zadi ya watu 400 wameuwawa na kundi la al- Shabab katika ardhi ya Kenya tokea Rais Uhuru Kenyatta aliposhika madaraka hapo mwezi wa Aprili mwaka 2013 wakiwemo 67 waliouwawa mwezi wa Septemba mwaka huo wakati wa kuzingirwa kwa jengo kuu la maduka katika mjii mkuu wa Nairob

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni