Watu 10
wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro baada ya kukamatwa msikitini
wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera nyeusi inayodaiwa
kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab wa nchini Somalia.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo, Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Leonald
Paul alisema tukio hilo limetokea juzi (Aprili 14 mwaka huu) majira ya
saa 3.30 usiku katika kitongoji cha Nyandeo, tarafa ya Kidatu wilayani
Kilombero.
Kamanda
Paul alimtaja mtu aliyefariki kuwa ni Hamad Makwendo ambaye umri wake
haujafahamika ambaye ni mkazi Manyasini Ruaha wilayani Kilombero.
Aidha
alisema siku ya tukio polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema
kuhusu watu hao na kwamba walitaarifiwa kuwa wanajihusisha na matukio
mbalimbali ya uhalifu na polisi waliamua kufatilia nyendo zao.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Paul alisema:
“Polisi
walipata taarifa kuwa watu hao walitumia usafiri wa bajaji mbili kwenda
kusikojulikana na wakati wakiendelea na zoezi la kufuatilia ndipo
walikutana na bajaji moja ikiwa na abiria mmoja ambaye ni Mkwendo na
kuisimamisha.”
Alisema
kuwa bajaji hiyo iliposimama marehemu huyo aliruka na kuanza kukimbia
ndipo askari mwenye namba F .3323 Koplo Nasoro alianza kumkimbiza na
alipomkaribia mtuhumiwa huyo alichomoa jambia alilokuwa nalo na kumkata
askari huyo eneo la shingoni.
Askari
mwingine mwenye namba E.9245 Koplo Chomola ambaye alikuwa nyuma
alifanikiwa kumpiga risasi ya mguu mtuhumiwa huyo, ambapo alipoanguka
chini wananchi wa eneo hilo tayari walifika katika eneo hilo na kuanza
kumshambulia marehemu huyo kisha kumchoma moto kwa hasira.
Kamanda huyo alisema walianza kuwasaka watu wengine ambao walipata taarifa wapo katika Msikiti wa Suni uliopo Kidatu.
“Polisi
walipofika katika msikiti huo waliuomba uongozi wa msikiti huo kuwatoa
watu wote waliokuwa msikitini ili kuweza kubaini watu ambao wanatiliwa
mashaka,”
Alisema polisi waliendelea na ukaguzi na kuwakamata watu hao 10 wakiwa na vifaa hivyo na kuwatia nguvuni.
Kamanda
huyo alitaja vitu vilivyokutwa katika mabegi yaliyokuwa ndani ya msikiti
huo ni pamoja na milipuko 30, bendera nyeusi yenye maandishi ya Kiarabu
yakisomeka ‘Mungu Mmoja’, majambia, bisibisi, vinyago vya kuziba uso
(masks), nguo za jeshi, misumeno ya chuma na spana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni