Ijumaa, 29 Mei 2015
MAAFISA WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI (NEC) WAVAMIWA NA KUJERUHIWA NA MAJAMBAZI MOMBA MKOANI MBEYA.
Picha ya maktaba mwanaume akiwa ameshika panga.
Wakati wananchi wakilalamikia uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo mpya wa kielektroniki wa Biometric Voters Registration (BVR), maofisa 10 wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) wameshambuliwa na kujeruhiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakati wakienda kuandikisha wapigakura wilayani Momba, mkoani Mbeya.
Walikumbwa na mkasa huo katika msitu wa Nyimbili, wakiwa njiani kutokea katika kata ya Chitete walikokuwa wanaandikisha wapigakura.
Mbali ya maofisa hao, dereva wa gari la halmashauri ya wilaya hiyo, Pius Kajula (47) ambaye ni mkazi wa Kamsamba, alijeruhiwa vibaya katika tukio hilo.
Akizungumza na NIPASHE akiwa wodini katika Hospitali ya Serikali Mbozi, Kajula alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku wakiwa njiani kutoka katika kijiji cha Chilulumo kuelekea kijiji cha Chitete baada ya kumaliza kuandikisha kata za Chilulumo, Ivuna na Mkomba.
Alisema saa 2:30 usiku akiwa anaendesha gari katika msitu huo ambao ni mkubwa na wenye kona nyingi, ghafla alikuta barabara imefungwa kwa magogo.
Alisema baada ya kuona hali hiyo alitambua kuwa kuna jambo la hatari na alipoanza kurudi nyuma ili kutafuta mwanya wa kugeuza gari kurudi walikotoka ili kuokoa maisha yake na aliowabeba walijikuta wameshazungukwa na watu hao.
Alisema akiwa kwenye harakati hizo, lilitokea kundi la watu kutoka ndani ya msitu huo wakiwa na mapanga na marungu na kuwaamuru waliokuwa ndani ya gari hilo kushuka.
Kajula alisema alijitahidi kupambana nao ili kuokoa maisha yao lakini ilishindikana na watu hao walianza kupiga gari hilo kwa mawe na kuvunja vioo vyote.
Alisema kutokana na mashambulizi hayo alilazimika kusimamisha gari na kuwaeleza maofisa hao washuke ili kujinusuru.
Alisema wakiwa wanashuka, watu hao walianza kuwashambulia kwa silaha hizo na katika harakati za kujiokoa alijeruhiwa kwa kukatwa mkono wa kulia na kichwani.
Alisema watu hao waliwaamuru kulala chini na kuwapekua na kuwapora vitu mbalimbali, ikiwamo simu na Sh. 175,000 taslimu.
Kajula alisema baada ya uporaji huo, watu hao walitoa magogo barabarani na kumlazimisha kuondoa gari ambalo aliendesha kwa mkono mmoja hadi Kituo cha Polisi Itaka kabla ya kwenda hospitali kwa matibabu.
Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Mbozi, Tulakela Kilatu, alisema majeruhi wote walipokelewa katika hospitali hiyo juzi majira ya saa 9:00 usiku na kutibiwa kabla ya kuruhusiwa isipokuwa dereva huyo.
Aliwataja majeruhi ambao walitibiwa na kuruhusiwa kuwa ni Diana Mlelwa (22), Sophia Msigwa (23), Henry Sichone (50), ambao ni wakazi wa Vwawa, Grace Mapunda (26), Irene Kajula (20), wakazi wa Ichenjezya na Ester Msukwa (27).
Wengine ni Amiri Msuya (34), ambaye ni mkazi wa Chitete, Alfred Simpol (28), mkazi wa Vwawa na Green Mwaigunde (51), mkazi wa Ichenjezya, Frobi Mnale (24), mkazi wa Tunduma na Mariam Simwingwa (23), mkazi wa Ichenjezya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, Anton Mwantona, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kitendo hicho hakivumiliki na kuomba vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka watu hao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Nyigesa Wankyo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea.
KIGOMA WAILALAMIKIA NEC
Zaidi ya wananchi 300 wa mtaa wa Masanga Rubabi, kata ya Buahanda, Manispaa ya Kigoma/Ujiji wameilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwa kukitengea kila kituo siku saba pekee, huku ikiacha idadi kubwa ya wananchi wakiwa hawajaandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akizungumza na NIPASHE jana kwa niaba ya wenzake, Obedi Mwanuzi (40), ambaye ni mkazi wa Mwasenga, alisema watu ni wengi na mashine ni chache.
Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakilala katika kituo hicho kila siku tangu mchakato huo uanze Mei 21, mwaka huu ili kupata fursa ya kujiandikisha kutokana na watu wanaojitokeza kuwa wengi.
Mkazi wa Mwasenga, Sadati Musa (38), alisema hali hiyo ilitokana na mashine kugoma.
Msimamizi Msaidizi wa kituo cha kata ya Buhanda, Sufiani Baruani, alisema kituo hicho kimekuwa na watu wengi kuanzia Mei 21, huku mashine ikiwa ni moja.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Mhandisi Weransari Moses, alisema wameona tatizo katika kituo cha Masanga Rubabi na kulazimika waongeze siku moja ili kumaliza kuwaandikisha watu waliosalia.
DK. MBASSA: UANDIKISHAJI UNA MIZENGWE
Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Dk. Antony Mbassa (Chadema), ameitaka serikali kueleza kwa nini uandikishaji katika daftari hilo umekuwa na mizengwe na kusababisha wananchi kukata tamaa.
Alitoa kauli hiyo jana bungeni alipoomba mwongozo akitaka kujua hatma ya uandikishaji, ambao unaonekana kujawa na mizengwe katika maeneo mbalimbali.
Alisema wananchi wamekuwa wakifukuzwa na watendaji, huku baadhi ya vifaa vikihamishwa bila kujali kuwa hawajaandikishwa.
Pia alitaka kujua kama serikali ina mpango wa kuongeza muda wa uandikishaji kutokana na muda unaotumika kuwa mchache huku changamoto zikiwa nyingi katika mchakato huo.
Akijibu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, Jenister Mhagama, alisema serikali imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wabunge na kukemea watendaji kuwanyanyasa wananchi kuwafanya washindwe kujiandikisha katika daftari hilo.
Alisema serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na baadhi ya wabunge na wananchi.
BAHI WALALAMIKIA UANDIKISHAJI KUSUASUA
Wakazi wa wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma wamelalamikia kusuasua kwa mchakato wa uandikishaji wa daftari hilo na hivyo kusababisha idadi kubwa ya watu kukosa fursa hiyo kutokana na uhaba wa BVR.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika vituo mbalimbali, walidai mchakato huo uliotarajiwa kumalizika jana katika wilaya hiyo, watu wengi watakosa kujiandikisha kutokana na uhaba wa BVR.
Yunge Ngalasho, mkazi wa kijiji cha Bahi Makulu, alidai mchakato huo umekuwa mgumu kutokana na changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza kutokana na BVR kuharibika mara kwa mara.
Rabeka Kusenha alisema kama serikali haitaongeza maofisa uandikishaji na BVR, watu wengi watakata tamaa na kuondoka kwenda kufanya shughuli zao nyingine za kiuchumi.
Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Bahi, Marthias Lyamunda, alisema kutokana na hali ilivyo katika vituo vya kuandikisha wapigakura kuna kila sababu ya kuongezwa muda katika wilaya hiyo.
Imeandikwa na Bosco Nyambege, Momba; Paul Mabeja, Bahi; Jacqueline Massano, Dodoma na Joctan Ngelly, Kigoma. CHANZO: NIPASHE
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni