Ijumaa, 29 Mei 2015

SIKU TATU ZA KISHINDO: 5 WATATANGAZA NIA

 
Na Boniface Meena, Mwananchi
  • CCM ipo kwenye wakati mgumu wa kutafuta mrithi wa Jakaya Kikwete katika nafasi ya urais na mwenyekiti wa chama hicho kikongwe nchini baada ya Rais huyo wa sasa kuongoza nchi kwa vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja na hivyo kulazimika kuondoka Ikulu kutokana na utashi wa kikatiba.


Dar es Salaam. Ni siku tatu za hekaheka na kujenga hoja za kujinadi kuanzia kesho wakati makada wa CCM watakapotangaza kwenye mikutano ya hadhara sababu zilizowasukumu kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CCM ipo kwenye wakati mgumu wa kutafuta mrithi wa Jakaya Kikwete katika nafasi ya urais na mwenyekiti wa chama hicho kikongwe nchini baada ya Rais huyo wa sasa kuongoza nchi kwa vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja na hivyo kulazimika kuondoka Ikulu kutokana na utashi wa kikatiba.
Kutokana na hilo, zaidi ya makada 20 wanatajwa kuwa na nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais ili kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano na watatakiwa kutangaza, kuchukua fomu na kuzirudisha ndani ya takribani siku 32 kabla ya Julai 2 ambayo ni siku ya mwisho iliyowekwa na chama hicho.

Kwa mujibu wa ratiba za makada wa CCM, kesho Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa atafanya mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kutangaza rasmi nia ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo ya juu nchini.

Habari ambazo Mwananchi imezipata kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa kumekuwa na maandalizi ya hali ya juu jijini Arusha kuelekea siku ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasili kwa watu mbalimbali wanaomuunga mkono wakiwamo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.
Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli, alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, lakini akalazimika kujiuzulu mwaka 2008 baada ya Kamati ya Bunge kuibua kashfa ya kuingia mkataba wa ufuaji umeme wa dharura na kampuni iliyokuwa haina sifa ya Richmond RDC, uamuzi ambao anasema aliufanya ili kuiokoa nchi.

Makada waliotangaza kuwa watatoa kauli ni mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya watakaotangaza Juni Mosi (Jumatatu) kila mmoja katika eneo lake. Makongoro inaeleza kuwa mtoto huyo wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, atatangaza nia yake akiwa kijijini kwao Butiama mkoani Mara.

Profesa Mwandosya, mbunge wa Rungwe Mashariki (CCM) ameeleza kuwa atatangaza nia yake Juni Mosi akiwa mkoani Mbeya na siku mbili baadaye atachukua fomu.

Wengine wawili ambao nao watatangaza nia siku moja katika maeneo tofauti ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Wasira, ambaye ni mbunge wa Bunda, ameeleza katika ukurasa wake wa Facebook kuwa atatangaza nia yake akiwa mkoani Mwanza keshokutwa (Mei 31) huku Mwigulu akitangazia nia yake mkoani Dodoma siku hiyohiyo.
Wasira, mbunge wa Bunda na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, amekuwa mbunge na waziri kuanzia mwaka 1970 na ndiye mwanasiasa mkongwe kuliko wote wanaotajwa kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Nchemba, ambaye ni mbunge wa Iramba Mashariki, alitangaza kujivua nafasi yake ya naibu katibu mkuu wa CCM-Bara ili ajikite zaidi kwenye harakati za kuwania urais.
Naibu waziri huyo wa fedha anatumikia kipindi chake cha kwanza bungeni.
Wakati makada hao wakijipanga kuwaeleza wananchi sababu zilizowasukuma kuomba kushika nafasi hiyo ya juu kisiasa nchini, makada wengine wa CCM bado hawajatangaza ratiba zao, huku baadhi wakiwa wameshatangaza nia na kwa sasa wanasubiri kuchukua fomu na baadaye kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, pamoja na waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ni miongoni mwa makada ambao hawajaweka bayana ratiba zao, ingawa Membe ameweka bayana kuwa atafanya hivyo kijijini kwake Mtama mkoani Lindi
Wengine ni mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, Mbunge wa Songea (CCM), Dk Emannuel Nchimbi, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Ambao tayari walishatangaza nia zao za kuomba kuteuliwa na CCM ni Pinda, Lazaro Nyalandu, ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Januari Makamba (Sayansi na Teknolojia), na Dk Hamisi Kingwangalla (mbunge wa Nzega).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni