Jumapili, 31 Mei 2015

MAJAMBAZI YAPORA SMG NA RISASI 30


http://world.guns.ru/userfiles/images/smg/smg14/hk_mp5a2.jpg
Watu 10 wanaosadikiwa ni majambazi wakiwa na mawe na mapanga wamemnyang’anya bunduki aina ya SMG na risasi 30, askari polisi wa Kituo cha Tazara kilichopo eneo la Yombo Station na kutokomea kusikojulikana.



Kamanda wa Polisi Kikosi cha Tazara Dar es Salaam, Patrick Byatao alisema Mei 27 mwaka huu saa 1:00 usiku, askari namba H.1574 PC Jineneko, alinyang’anywa SMG yenye namba 56-1402621 na risasi hizo huku majambazi hao wakimshambulia kwa mawe na mapanga.

Byatao alisema kuwa, siku ya tukio askari D.8386 SGT Juma na H.1574 PC Jineneko , walipangiwa kazi lindo la Yombo Station na kila mmoja alikuwa na silaha aina ya SMG na risasi 30.

Alisema askari hao waliacha lindo na kwenda kupata chakula cha jioni, jirani karibu na eneo hilo wakiwa wanakula ulitokea ugomvi kwenye duka la kuuza CD.

“Wakati ugomvi unaendelea ndipo wakaenda kuamulia, walifanikiwa kukamata watuhumiwa wawili, lakini kabla hawajachukua hatua yeyote walivamiwa na kundi la majambazi hao na kuwapora silaha hiyo, huku askari Jineneko akijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake na amelazwa katika Hospitali ya Temeke na anaendelea vizuri,” alisema Byatao.

Byatao alisema chanzo cha tukio hilo ni uzembe wa askari hao kuacha lindo na kwenda kupata chakula sehemu nyingine.

Alisema jeshi hilo linaendesha msako mkali kwa lengo la kupata silaha na watuhumiwa waliopora silaha hiyo iliyokuwa na risasi 30, huku wakiendelea kuwashikilia watu saba kuhusiana na tukio hilo.

“Hata hivyo, hadi sasa , silaha hiyo haijapatikana na jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na raia wema, vituo vya polisi na kikosi vilivyopo jijini humu na nje ya Dar es Salaam,” alisema Byatao.

Alisema wanaendelea na uchunguzi ili kuangalia chanzo cha tukio hilo huku akiwataka wananchi kutoa taarifa polisi kwa watu wanaomiliki silaha, kwani wakikaa kimya inaweza kutumika kuwadhuru, hata kuleta maafa.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo Abraham Salehe alisema waliwaona vijana hao wakiwa kwenye duka linalouza CD, ghafla walianza kugombana wakati wanagombana ndipo askari wawili waliokuwa eneo hilo walikwenda kwa ajili ya kuamulia.

Salehe alisema wakati wanafanya hivyo, ghafla lilitokea kundi kubwa na kumvamia mmoja wa askari hao kwa kumpiga kwa mawe na mapanga na kumpora silaha aliyokuwa nayo.

Wakati huo huo  watu 15 Wilayani Rufiji,wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za moto na mapanga wamevamia kituo kidogo cha Polisi Mloka, kilichopo tarafa ya Mkongo wilayani Rufiji wakiwa na lego la kuua askari na kupora silaha.

Majambazi hayo yalivamia kituo hicho usiku wa kuamkia juzi na yalirusha risasi hewani, kwa lengo la kuwatisha wananchi na askari wawili waliokuwepo kituoni hapo ili wasitoe upinzani wowote wakati wa uvamizi huo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Jafari Mohamed alithibitisha kuvamiwa kituo hcho usiku na watu hao wakiwa na mapanga kwa lengo la kufanya uhalifu.

Alisema kuwa kundi hilo la watu lilivunja mlango wa kituo hicho na kuingia ndani lakini hawakukuta silaha wala askari aliyekuwemo ndani na kwamba askari wote wako salama. Chanzo MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni