Jumapili, 31 Mei 2015
MLONGE : MTI WA DAWA NA BIASHARA
MLONGE kwa jina la kitaalam unajulikana kwa jina moringa oleifera. Mti huo wa kipekee ambao asili yake ni India, siku hizi unapandwa sehemu nyingi za kanda za kitropiki na nusutropiki.
Hapa nchini kuna miti ya aina mbalimbali ikiwemo ile inayotambulika na jamii kutokana na umaarufu na pia ipo ambayo haifahamiki kabisa.
Mfano wa miti inayofahamika kiasi kwamba hata ukiitaja katika kundi la watu wengi wao wanakuwa wanaifahamu ni pamoja na mti wa muarobaini na mbuyu, ambayo imekuwa ikifahamika kuwa ni miti dawa na imekuwa ni msaada mkubwa kwa wale wanaofahamu matumizi yake.
Miti mingine ambayo pia ni dawa ni ile ya aina ya mlonge ambayo inapokauka huweza kutumika kwa kuni. Si hivyo tu, inaaminika kwamba miti hiyo inatoa mkaa mzito na wenye kudumu kwa muda mrefu. Mti huo wa mlonge ambao pia ulifanyiwa utafiti kwa muda mrefu ni tiba nzuri kwa magonjwa mengi ya binadamu.
Licha ya mti huo kutibu magonjwa mbalimbali, mlonge pia ni dawa ya inayowekwa kwenye maji na kuua wadudu na kusafisha maji ya kunywa. Mbegu za mlonge zina uwezo wa kutibu baridi yabisi na uvimbe wa magoti, kifua kikuu (TB), kisukari , kuongeza kinga mwilini, kukosa usingizi, magonjwa ya zinaa, harufu mbaya mdomoni, vidonda vya tumbo, majipu pamoja na homa ya matumbo.
Magonjwa mengine yanayotibika kwa mbegu hizo ni malaria sugu, pumu, matezi, saratani na maumivu ya mwili. Mafuta ya mbegu hizo ni dawa ya kuchua maumivu ya mwili. Pamoja na hayo, gome la mlonge linapochemshwa na kulainika ni dawa ya ugonjwa wa bandama, ini, maumivu, tetenasi na kupooza.
Pia majani ya mlonge yanapopikwa huliwa na kusaidia katika kupambana na uhaba wa vitamin C kwani upungufu wa vitamini hiyo husababisha damu kuvuja kwenye fizi za meno. Hali kadhalika, majani ya mlonge yanapowekwa kwenye kidonda au uvimbe yanakuwa tiba nzuri kwa kidonda.
Juisi inayotokana na majani ya mlonge ikichanganywa na asali ni dawa nzuri kwa magonjwa ya macho. Pia majimaji ya majani ya mmea huo hurekebisha msukumo wa damu na kupunguza maumivu ya kichwa. Majimaji ya majani ya mlonge yanatumika kurekebisha kiwango cha sukari mwilini hasa kwa watu wenye tatizo la kisukari.
Mti huo pia unaongeza kinga ya mwili wa binadamu na majimaji ya majani yake yanatumika kwa dawa ya ngozi. Kwa mujibu wa wataalamu, mmea huo pia una kazi kubwa ya kupunguza uvimbe na maumivu ya viungo.
Wazazi wengi hulalamika kutoa maziwa machache ya kunyonya watoto lakini ni kwa sababu hawafahamu kwamba miti ya asili kama mlonge huweza kupunguza tatizo hilo. Kuna madai pia kwamba, mlonge unasaidia kupunguza maumivu yanayotokana na mafua makali na kupunguza kiwango cha kolestero mwilini.
Inaelezwa kuwa mbegu za mlonge zinaweza kutumika kutengeneza mafuta yenye ubora sawa na mafuta ya alizeti na mzeituni. Pamoja na mambo mengine, mti huo pia unaweza kutumika kutengeneza vipodozi, sabuni na mafuta.
Maua ya mlonge hutumika kutengeneza chai, na unga wa majani ya mlonge unapochanganywa na chakula huongeza nguvu mwilini. Mmea wa mlonge una kiwango kikubwa cha virutubisho vyenye manufaa kwa mwili wa binadamu na mifugo. Una virutubisho zaidi ya 90 na unaweza kutumiwa na watu wa umri wote bila ya kuwa na madhara yoyote ambayo yamethibitishwa na wataalamu.
Baadhi ya taasisi au vituo vinavyojishughulisha na masuala ya mimea wametambua umuhimu wa mmea hiyo na kutoa elimu ya matumizi, faida na changamoto za mti huo. Mti huo ambao una ukubwa kama wa mmea wa parachichi, ni rahisi kuanguka unaposukumwa na upepo mkali kwa kuwa ndani ya mti huo ni kama bua la mahindi na wenye maji mengi.
Mara nyingi hupandwa katika maeneo tofauti tofauti ambayo udongo wake huwa wenye rutuba kiasi, na kwamba mizizi yake hata ikikatwa huendelea kukuza mti huo. Mti huu una virutubisho na faida na kila kitu kinaweza kuwa na matumizi chanya kwa watumiaji wa mlonge.
Pia mlonge unaweza kupikwa na kuwa mboga na unaweza kukaushwa na kutumiwa kwa matumizi ya muda mrefu. Mti huo unaweza kukua na kuanza kutumika kwa kipindi kifupi na kabla ya kuvuna unaweza ukaanza kunufaika na majani na mbegu zake.
Kupitia mti huo unaweza kubadilisha maisha ya wengi kwani kwa sasa soko la mlonge ni kubwa nchini kuliko ilivyokuwa awali. Hata hivyo, awali Watanzania wengi walikuwa hawaelewi faida na matumizi ya mti huo na wengine walikuwa hawajui hata unafananaje.
Wataalamu wa tiba mbadala, Ideal Health Care wamejikita katika kutoa elimu ya ujumla namna na jinsi ya kupanda mti huo na pia ni wanunuzi mti huo. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Dk John Kabugi anasema endapo mti huo ukitumika vizuri utasaidia katika kuongeza pato la taifa kwa kuwa sasa wananchi wengi wamepata mwangaza kuhusu mti huo.
Dk Kabugi anasema, wameamua kupita mikoa mbalimbali nchini kutoa elimu kuhusu mti wa mlonge na manufaa yake yote ili wakulima na watu wote wanaootesha mti huo, wauelewe na wanufaike.
“Tumefanya semina na kutoa elimu katika mikoa mbalimbali na tumeweza kufanikiwa; kwani mwitikio wa watu ni mkubwa na tunaamini wakichukua elimu hii wanaweza kufanikiwa na kujipatia kipato kupitia mti huu,” anasema Dk Kabugi.
Anasema wameamua kuwafundisha wakulima kwamba mlonge ni biashara nyingine kwa sababu kila kipatikanacho katika mti huo ni biashara na lishe. “Sisi wenyewe tumeamua kuwa soko, tumeandaa semina ambayo tayari tumefanya katika mikoa mbalimbali jinsi ya kupanda mpaka kuvuna na kuuza mti huu na kupata faida ili kuliongezea taifa pato lake,”anasema.
Mti wa mlonge una soko kubwa si hapa nchini pekee bali hata nje ya nchi kwani huko watu wake wanaufahamu mti huo na umuhimu wake. ‘’Mti huu unaweza kupandwa popote kwani hauchagui mazingira na unakua kwa kipindi kifupi tofauti na miti mingine ambayo inatumia muda mrefu kukua,’’ anasema Dk Kabugi.
“Mti huu hauna jasho na ukipanda mmoja ukakua unaweza kupata miti mingi zaidi kwa kuwa inaweza kukua ukubwa wa kati na kuleta kivuli cha muda,’’anasema.
Anasema, kwa kuwa mti huo unakua haraka utamsaidia mkulima kujipatia fedha mapema kwa sababu ukianza kukua mpandaji anaweza kuanza kuuza majani kama mboga, au kukaushwa ili kupata unga huku akiendelea kusubiri mti ukue.
Hata hivyo anasema, wapandaji wa milonge waepuke kuuza milonge mizima nje ya nchi bila kubakisha chochote kwa kuwa kufanya hivyo ni kuwafanya wageni kuipeleka katika nchi zao na matokeo yake wanaleta bidhaa za mti huo kwa gharama kubwa.
“Kumekuwa na baadhi ya watu wanaopanda miti ya milonge lakini akija mgeni anamuuzia kila kitu hadi mizizi. Kitendo hicho kinachudumaza ukuaji wa mlonge huo kwa mara ya pili,” anasema. Chanzo HABARILEO
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Soko la mlonge na bei yake ni bei gani kwa kilo ya mbegu
JibuFuta