Jumatano, 25 Februari 2015

RAIA 100 WA ETHIOPIA JELA NCHINI KENYA

Raia mia moja wa Ethiopia wakifuatilia kesi yao mahakamani leo hii
Raia mia moja wa Ethiopia hii leo wamehukumiwa kifungo cha miezi kumi na mbili gerezani nchini Kenya au walipe faini ya takriban dola 600 baada ya kupatikana na hatia ya kuwemo Kenya kinyume na sheria.
Polisi waliwakamata wahamiaji wao haramu siku ya Jumatatu katika mtaa mmoja mjini Nairobi. Maryam Dodo Abdalla anaarifu zaidi.

Wahamiaji hao haramu walioonekana wachafu na waliodhoofika kwa njaa, walikiri mashtaka hayo baada ya kusomewa makosa yao mmoja baada ya mwingine na hakimu Victor Wakhumile mjini Nairobi.
Sasa wanatakiwa kutumikia kifungo hicho au walipe faini waliyotozwa, na baadaye watasafirishwa kurudishwa Ethiopia walikotoka.
Kwa kilio, wameielezea mahakama kwamba wamewasili Kenya wakiwa wanaelekea Afrika Kusini ambako wameahidiwa kupewa ajira.
Polisi nchini Kenya iliwanasa raia hao mia moja wa Ethiopia, mapema wiki hii wakiwa wamehifadhiwa katika chumba kimoja kidogo, eneo la Embakasi mjini Nairobi.
Mkuu wa kitengo maalum cha kuzuia uhalifu nchini, SCPU, Noah Katumo amesema kwamba waliwakamata baada ya kupata fununu kwamba kuna wageni wengi waliowasili katika mabasi mawili tofuati kutoka Ethiopia katika mtaa huo.
Raia mia moja wa Ethiopia hii leo wasikitika na wengine wakilia mahakamani kufuatia hukumu ya kifungo cha miezi kumi na mbili gerezani nchini Kenya au faini ya takriban dola 600 za Kimarekani
Miezi kadhaa ya nyuma, wahamiaji wengine zaidi ya mia moja kutoka Ethiopia walihukumiwa kwa makosa kama hayo ya kuwepo Kenya kinyume cha sheria na walihukumiwa miezi sita gerezani.
Ni wahamiaji wengi haramu wanaovuka mpaka na kuingia Kenya kutoka Ethiopia.
Wengi huitumia Kenya miongoni mwa nchi nyingine kama Tanzania, Msumbiji Malawi na Zambia kama njia ya kupita kuelekea Afrika kusini.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kimataifa la wahamiaji, IOM, kuwa wahamiaji 17,000 hadi 20,000 wanaelekea Afrika kusini kila mwaka.
Asilimia 60 ya idadi hii ni wanaume kutoka Ethiopia wanaohadaiwa kwamba watapata ajira na maisha mazuri.
Katika mahakama hiyo hiyo leo, raia watatu wa Kenya wameshtakiwa kwa makosa ya kuwasafirisha kiharamu raia hao 100 wa Ethiopia.
Hata hivyo wamekana mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya takriban dola 950 na kesi yao sasa inatarajiwa kutajwa tena tarehe 11 mwezi Machi 2015

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni