Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo, akitangaza nia ya kuwania
urais kupitia CCM katika mkutano uliofanyika Mjini Musoma jana. Picha
na Peter Saramba
Dar es Salaam. Mbunge wa kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo ameeleza jinsi atakavyoondoa umaskini nchini kwa kutumia uchumi wa gesi endapo atapitishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwania urais.
Akitangaza nia ya kuwania nafasi hiyo mjini Musoma jana, Profesa alisema: “Nitafuta umaskini kwa kutumia uchumi wa gesi ambao utakuwa unamilikiwa na Watanzania wenyewe… gesi nimesomea kwa hiyo ninafahamu mambo haya vizuri.
“Tena kutokana na juhudi zangu za kuhamasisha vijana wapelekwe nje kusoma masomo ya gesi, nategemea mwakani tutakuwa na wataalamu wengi zaidi watakaoweza kufanya kazi kwenye sekta hii. Lakini pia hata baadhi ya vyuo vikuu nchini kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dodoma vimeanzisha shahada za masuala ya gesi kwa hiyo kadri tunavyoendelea, tutakuwa na wataalamu wa kutosha.”
Profesa Muhungo aliyekuwa ameongozana na mkewe, Bertha Mamuya alisema ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, kutakuwa na mfuko maalumu kwa ajili ya kutunza fedha za gesi... “Matumizi ya mapato ya gesi yatakuwaje?” alihoji na kuendelea kutoa ufafanuzi wake kwa makini.
“Mapato ya gesi hayatakwenda Hazina. Tutafungua mfuko maalumu kwa ajili ya kutunza fedha hizo. Kama ikitokea kiasi fulani kinahitajika kwa ajili ya matumizi fedha zitakuwa hazitoki hivihivi tu.
“Kila mwaka Bunge litakuwa linajadili tutoe kiasi gani kwenye mfuko ili kiweze kusaidia kwenye matumizi hayo. Lakini kabla ya kutolewa, pia kwenye mfuko huo nitakaouanzisha, kwa mara ya kwanza, lazima ridhaa hiyo itoke kwa Watanzania wenyewe.”
Profesa Muhongo ambaye alitumia kaulimbiu ya ‘Tukuze uchumi, tuondoe umasikini’, alisema: “Mfuko huo kwa mara ya kwanza utatumika kutoa mikopo nafuu ya riba ndogo kwa Watanzania wanaofanya shughuli zao kwenye sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji na michezo. Watakuwa wanapata mkopo wa riba ya asilimia mbili… haya yote yatakuwa yanapitishwa na wabunge kwa ridhaa ya wananchi.
“Tutatunga sheria kwa ajili ya kusimamia mipango yote hii… tutageuza uchumi wetu kupitia uvuvi, kilimo, michezo na ufugaji kutoka asilimia saba hadi asilimia15 ifikapo 2025.” Profesa Muhongo alisema uchumi wa gesi utaongeza uzalishaji wa umeme zaidi tofauti na unaozalishwa sasa kwa ajili ya matumizi ya viwanda na majumbani ambao ni Megawati 1,500 tu.
“Gesi itasaidia kuongeza uzalishaji wa umeme utakaokuwa unatumika viwandani. Uzalishaji huo utaongeza ajira kwa vijana pia.”
Mbali na gesi, katika hotuba yake ya saa 1.05, Profesa Muhongo alisema, amefanya utafiti katika maeneo mbalimbali na kubaini kuwa Tanzania bado ina hazina kubwa ya madini ambayo hayajachimbwa.
“Nafahamu... sidhani kama kuna mtu mwingine anafahamu kama mimi. Mkinipa ridhaa yenu wanaCCM, nitahakikisha tunatumia vyema fursa hizo kwa ajili ya manufaa ya uchumi wa Taifa hili,” alisema.
Kuongoza kisomi
Profesa Muhongo alisisitiza kuwa akipewa dhamana, ataunda Serikali ya kisomi ambayo itatekeleza majukumu yake kwa kutegemea tafiti mbalimbali za kisayansi. Alisema Serikali zote katika nchi zilizoendelea zinafanya hivyo.
Alisema nchi inayoongoza kwa kuwa na watafiti wengi duniani ni Finland, ambayo ina watafiti 7,707 katika watu milioni moja. Alisema utafiti ndiyo umeufanya uchumi wa nchi hiyo kuwa imara.
Alisema Tanzania haiwezi kujenga uchumi kama hakuna wataalamu wa kutosha watakaojua rasilimali zilizopo nchini na kuelewa namna ya kuzitumia ili ziwanufaishe Watanzania wote.
“Mtu wa kufanya yote haya ndani ya CCM ni mimi, mnanijua vizuri, sina ubabaishaji kwenye mambo muhimu ya maendeleo. Naomba kupewa dhamana hii ili kukuza uchumi wa nchi yetu na mtu mmojammoja,” alisema Profesa Muhongo.
Moja ya mipango yake ya kutokomeza umaskini ni kuwekeza katika elimu. Katika eneo hili alisema, atahakikisha vifaa vya elimu vinapatikana shuleni na masilahi ya walimu yanaboreshwa. Alitolea mfano wa nchi ya Finland kwamba inawalipa walimu mishahara sawa na madaktari.
Profesa Muhongo alisisitiza kuwa utafiti ni jambo muhimu katika utawala na biashara za kawaida. Alisema mfanyabiashara anaweza kufanya utafiti mdogo wa kutaka kujua bidhaa gani inanunuliwa zaidi sehemu fulani ili kuifanya kwa ufanisi.
“(Said) Bakhresa anauza sana kwa sababu anafanya utafiti, kabla ya kutengeneza bidhaa. Nchi ikiendeshwa kwa tafiti tutapata maendeleo kwa haraka na kufikia lengo la kuwa nchi yenye uchumi wa kati miaka 10 ijayo,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza:
“Mfanyabiashara anayepanga lazima ajue nchi ina watu wangapi na dunia ina watu wangapi ili ajue auze huko kiasi gani cha korosho, pamba au kahawa anayozalisha. Wote wakifanya hivyo, uchumi wetu utakua kwa kasi.”
Changamoto
Profesa Muhongo alisema tangu nchi inapata uhuru, ilikuwa na maadui watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi, wakati huo ikiwa na watu milioni tisa, lakini kufikia Mei, kuna watu milioni 49.5 na matatizo hayo bado ni sugu.
Alisema ongezeko hilo la watu limesababisha changamoto nyingine ambazo atakabiliana nazo. Alizitaja kuwa ni rushwa, ukosefu wa ajira kwa vijana, siasa kila mahali, uonevu na dhuluma.
Changamoto nyingine alizitaja kuwa ni kutojiamini kwa Watanzania, uvivu na utegemezi, kutopatikana kwa takwimu sahihi na kupungua kwa amani, utulivu, upendo na usalama wa Taifa. Alijigamba kuwa kwa elimu yake, anajiamini na ana uwezo wa kufanya hayo.
“Kiongozi lazima awe na maono na kujua namna ya kutekeleza maono yake. Vipaumbele vyangu ni kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuondoa umaskini. Hakuna mtu mwingine anayeweza kufanya haya ndani ya CCM, ni mimi tu,” alisema Profesa Muhongo, huku akishangiliwa na mashabiki wake waliohudhuria hafla hiyo.
Hali iliyokuwa
Watu wa hali ya kawaida mjini Musoma ndiyo waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza Profesa Muhongo. Walioonekana kuwa na uwezo walitumia pikipiki kufika eneo alilotangazia nia.
Waendesha pikipiki, maarufu bodaboda, walifaidi matunda ya mkutano huo kutokana na kupata abiria wengi kutoka viunga vya mji wa Musoma kuwapeleka wananchi katika Ukumbi wa MCC ilikofanyika shughuli hiyo.
Hata hivyo, shughuli hiyo ya Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, iliingia doa baada ya umeme kukatika saa sita mchana na kusababisha malalamiko kwa baadhi ya wananchi, baadhi wakidai kwamba ni hujuma ya washindani wake.
“Nchi hii ni hatari wameona anatangaza jembe wakakata umeme ili tusimshuhudie,” alisikika mtu mmoja akilalamika eneo la Bohari Kantini.
Umeme huo ulirejea saa 9.15 alasiri kwa dakika kadhaa na kukatika tena ilipotimu saa 9.33 alasiri. Baadaye saa 9.55 alasiri ulirejea.
Hali hiyo ilionekana dhahiri kumkera Profesa Muhongo ambaye kwenye hotuba yake alisema alipokuwa waziri wa wizara hiyo, wananchi walisahau kukatika kwa umeme.
Hata hivyo, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mara, Henry Byabato alisema umeme ulikatika mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana na hitilafu hiyo iliyotokea kwenye Gridi ya Taifa.
Profesa Muhongo ambaye aliingia ukumbini akiwa ameongozana mkewe, Bertha na mfanyabiashara maarufu mjini hapa, Dora Jama na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Daud Misango huku akishangiliwa, alisema muda huu siyo wa kutukanana au kulaumiana kwa sababu mambo hayo hayaondoi umaskini wa Watanzania.
Kama kawaida yake, alikuwa na vibwagizo, kimojawapo kikiwa ni juu ya wasifu wake akisema hana haja ya kuelezea kiwango chake cha elimu, kwani anaweza kutumia muda mrefu, bali kama ni kusoma amesoma na utaalamu wake umefikia hatua ya mwisho.
Atangaza nia
Akitangaza nia yake hiyo, Profesa Muhongo alitaja vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na mtazamo mpya, maono ya mbali, mabadiliko, msimamo usioyumbishwa, uzoefu na mafanikio.
Alisema ana uhakika wa kuyasimamia hayo kwa kuwa ni mchapakazi mwenye kuaminika aliye na utaalamu na ujuzi wa hali ya juu, mzoefu wa kimataifa, mkweli, mwaminifu, mwadilifu, mzalendo wa kweli, mtu wa uamuzi wa busara na mwenye uwezo wa kusimamia ilani.
“Nia yangu ni kuomba ridhaa ya wanaCCM, tusifanye sherehe, sikuja hapa kumsema mtu kwa sababu hata ukimsema umaskini wa watu wetu bado upo palepale… mimi nimekuja na suluhisho la kuwaondolea umaskini Watanzania,” alisema Profesa Muhongo.
Kama kawaida yake anapokutana na watu, aliwataka wananchi wenye kalamu na karatasi kuanza kuandika takwimu kwa sababu hazungumzi bila utafiti... “Nilikata kadi ya Tanu mwaka 1975 nikiwa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) na mwaka 1977 nikakata ya CCM na risiti zote ninazo hizi hapa (huku akizionyesha kwa wananchi), hivyo ni mwasisi wa CCM, kama naweza kutunza hivi, basi mimi ndiyo nafaa kutunza rasilimali zenu.” Alisema hafanyi kampeni za urais, bali anachohitaji ni kupewa ridhaa ya chama ili kupeperusha bendera yake, huku akikataa kuahidi chochote kwa sababu hawezi kuahidi kujenga shule au kupandisha mishahara bila kukuza uchumi ambao ndiyo kazi yake kuu.
Profesa Muhongo alisema Watanzania pia wanakabiliwa na tatizo la kupungukiwa ushindani kuanzia katika michezo, ajira na soko la kimataifa kutokana na kutojiamini hata kwa mambo wanayoyajua na kuyamudu vyema.
“Ajira za ndani na nje tunalalamika tu ooh..fulani anatuchukulia kazi zetu na hata kwenye masoko tuko nyuma sana kama Taifa. Anayetaka kuongoza Tanzania lazima ajue mambo haya na awe na maono ya kukuza ya uchumi, kuondoa umaskini, kuongeza uzalishaji na kuongeza uwezo wa kujitegemea wa watu binafsi na Taifa,” alisema.
Usomi wake
“Itoshe tu kusema kama ni kusoma nimesoma hadi mwisho wa kisomo kinapoishia. Nikieleza utaalamu ambao unaanza baada ya kisomo pia nimefika hadi mwisho wa utaalamu unapofikia,” alisema mtaalamu wa Jiolojia.
Alisema katika maisha yake ya utaalamu, amefanya utafiti na wataalamu wa Ujerumani kwa miaka 30 na wenzake wa Uingereza kwa zaidi ya miaka 20 huku akifanikiwa kupanda ngazi ya juu katika vyama vya wataalamu wa jiolojia Marekani, China na Uingereza.
Alijigamba kwamba hata mkewe Bertha aliyemtambulisha kwenye mkutano huo, ni mwanasayansi ya Kemia na iwapo atafanikiwa kuwa rais, Taifa hili litaongozwa kwa mara ya kwanza na wanasayansi.
Imeandikwa na Midraj Ibrahim, Florence Focus, Peter Saramba, Veronica Modest, Suzan Mwillo na Peter Elias.MWANANCHI

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni