Leo
ni siku inayofuatia jana, siku ambayo Ndugu yangu Edward Ngoyai Lowassa
aliacha rasmi uanachama wa CCM na kupewa kadi ya uanachama wa Chadema.
Si yeye tu bali alisindikizwa na mke wake mpendwa Mama Regina Lowassa.
Nilidhani
leo mitandao yote ingesheni habari hiyo kubwa. Kumbe nami nimekuwa
"staa" katika mitandao ya kijamii. Kuanzia asubuhi nimekuwa nikipokea na
kujibu simu mbalimbali nikiulizwa maoni yangu kuhusu tukio la jana,
kuhusu mchakato wa Dodoma uliomalizika hivi karibuni, na "habari" kubwa
imekuwa Mwandosya, Mwapachu na ole Medeye wahamia Chadema!
Kuhusu Ndugu Lowassa kuhamia Chadema nionavyo mimi ni jambo la kawaida sana katika demokrasia ya vyama vingi.
Wanachama
hutoka na kuingia karibu kila siku. Hivyo basi tukio la jana
lisingegonga vichwa vya habari kama isingekuwa kwa umaarufu wa mhusika.
Jambo la msingi kwa CCM ni kutafakari, bila ghadhabu, na kwa utulivu, ni
sababu zipi za msingi zilizofanya hili jambo litokee? Je tunaweza
kujifunza lolote katika hili ili kukiimarisha Chama? .
Tunaweza
kuboresha nini katika taratibu na kanuni zetu? Nimeulizwa pia kitendo
cha Ndugu Lowassa kuhamia Chadema kina athari gani kwa CCM? .
Pamoja
na kutotokuwa msemaji rasmi wa Chama, tukio hili lina maslahi ya umma
kwa ujumla hivyo kukwepa kujibu hakusaidii. Siasa ni takwimu, hasa
tunapoelekea Oktoba. Kwa mantiki hiyo mtu mmoja kukihama Chama kuna
maana kura moja iliyopungua.
Kwa
kuwa haiwezekani kuirudisha, basi changamoto ni kuwa na mkakati wa
kutafuta kura ya kufidia, kuzuia kupotea kwa kura nyingine, na kuongeza
idadi ya wanaoingia ili iwe kubwa kuliko ile ya wanaotoka.
Msaafu
wa dini unasema mchungaji bora ni yule anayeweza kuwaacha kondoo wake
tisini na tisa walio salama ili amtafute yule mmoja aliyepotea! Suala la
kujiuliza katika mazingira ya yaliyotokea ni je tulikuwa wachungaji
bora? .
Nadhani
moja ya mambo ya msingi CCM itabidi tulitafakari kuhusiana na mchakato
wa kumpata mgombea wetu kwa nafasi ya urais ni je tunamtafuta mwanachama
ambaye atakuwa Rais? Je tunamtafuta mtu ambaye atakuwa Rais wa nchi na
Mwenyekiti wa Chama? Au tunamtafuta mtu atakayekuwa Rais na Waziri
Mkuu?
Vigezo
vya kumtafuta mtu huyo vinapishana kama ambavyo orodha wa wenye nia au
mifumo ya kumpata itapishana. Naamini tungelitafakari haya yote huenda
tusingefika hapa tulipo. Lakini Taifa ni kubwa kuliko sisi watu na uhai
wake ni mpaka "kiama cha wafu".
Tujadili
masuala haya na mengine muhimu, kwa ujasiri, uwazi na ukweli.
Nahitimisha kwa kujibu taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii
na watu wengi ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari kuhusu Mwandosya
kuhama kwenda Chadema.
Misingi
iliyojengwa na waasisi wa Chama, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume naendelea kuamini bado ni
sahihi. Ndiyo iliyotuletea heshima kubwa kama Taifa.
Kama
tumeyumba turudi katika misingi. Itikadi ya Chama inajengwa juu ya
misingi hiyo. Hivyo basi kwangu mimi Ilihali misingi ipo, na imara,
nitaendelea kuwa mwanachama wa CCM ili kwa pamoja na wanachama wenzangu
tuendelee kulijenga Taifa juu ya misingi hiyo, kila wakati tukikumbuka
kile alichotuasa Baba wa Taifa, Tujisahihishe! Prof.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni