Alhamisi, 14 Julai 2016

THERESA MAY AANZA KUIONGOZA UINGEREZA KAMA WAZIRI MKUU

Waziri mkuu mpya wa Uingereza Theresa May ameanza rasmi jana kushika hatamu za kuiongoza nchi hiyo inayojitoa kutoka Umoja wa Ulaya. Lakini ameanza kwa mbinyo mkubwa kutokana na uteuzi wa baraza lake la mawaziri.
Großbritannien Theresa May Downing Street 10 Waziri mkuu mpya wa Uingereza Theresa May
Uteuzi huo ikiwa ni pamoja na kumteua Boris Johnson kuwa waziri wake wa mambo ya kigeni. Huyo ni waziri mkuu Theresa May alipoanza kwa mara ya kwanza kutoa tamko lake rasmi baada ya kuombwa na malkia Elizabeth kuunda serikali, baada ya chama chake cha Conservative kumteua kuwa waziri mkuu badala ya David cameron.
Großbritannien Theresa May Downing Street 10 Theresa May akiwa na mume wake Philip
Wiki tatu baada ya Uingereza kupiga kura kujitoa kutoka katika Umoja wa ulaya, May pia anajikuta katika mbinyo mkali kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya , ambao wanamtaka kuanzisha mchakato wa kujitoa haraka iwezekanavyo.
Na wakati hali isiyoeleweka ya kiuchumi ikiongezeka kutokana na mshituko wa uamuzi wa kujitoa kutoka kundi hilo la mataifa, Benki ya Uingereza ilikuwa inatafakari uwezekano wa kupunguza riba ili kuchochea uchumi. Waziri mpya wa fedha ni waziri wa zamani wa mambo ya kigeni Philip Hammond.

Großbritannien Kabinett Philip Hammond Philip Hammond waziri mpya wa fedha
Uhusiano mwingine na Umoja wa Ulaya
Akionekana kuwa mtu makini ambaye alifanya kampeni upande wa kuibakisha Uingereza katika Umoja wa Ulaya, May aliingia madarakani akiahidi , kuiweka Uingereza katika nafasi muhimu nje ya kundi hilo la mataifa.
Lakini uteuzi wake katika kikosi chake cha karibu katika uongozi wake umezusha mshangao, ikiwa ni pamoja na meya wa zamani wa London Boris Johnson kuwa waziri wa mambo ya kigeni na mwanadiplomasia wa siku nyingi na mtu ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitia shaka kuhusu Umoja wa Ulaya David Davis akikabidhiwa wadhifa muhimu wa mchakato wa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya.
Viongozi wa Ulaya, wakiwa bado wanatikisa vichwa kutokana na uamuzi wa Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya katika historia yake ya miaka 60, wanamuwekea mbinyo May kuchukua hatua za haraka kuvunja ndoa hiyo.
Großbritannien Theresa May und Boris Johnson Boris Johnson (kushoto) waziri mpya wa mambo ya kigeni akiwa na waziri mkuu Theresa May (kulia)
Kuhusu hilo May alisema "Kufuatia kura ya maoni, tunakabiliwa na muda wa mabadiliko makubwa nchini mwetu na nafahamu kwa sababu hii ni Uingereza kuu tutafanikiwa. Wakati tunaondoka kutoka Umoja wa ulaya, tutaweka uhusiano bora zaidi duniani na tutaifanya Uingereza kuwa nchi ambayo haifanyi kazi kwa ajili ya watu wachache lakini kwa kila mtu."
Deutschland CDU-Wahlkampfveranstaltung in Zingst Angela Merkel Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Viongozi wa Ulaya
Kura hiyo ya maoni, imetengeneza hali mpya ambayo Uingereza na Umoja wa Ulaya zitalazimika kuangalia hivi karibuni, amesema rais wa Umoja wa Ulaya Jean-Claude Junker katika barua kwa May iliyochapishwa pia katika ukurasa wa Twitter.
Mazungumzo ya kwanza ya simu ambayo May aliyafanya ni pamoja na viongozi wa mataifa makubwa mawili ya Ulaya, kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francois Hollande. kansela Merkel amemwalika May kutembelea Ujerumani na ameelezea matumaini yake kufanya naye kazi, amesema hayo wakati akiwa ziarani nchini Kyrgyzstan leo Alhamis.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre
Mhariri: Mohammed Khelef
Chanzo: DW

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni