Ninamkuta Wilson akiwa amelala kwenye godoro. Anageuza shingo taratibu kuniangalia. Ninapo mwita na kumsalimia nikitaka kujua anaendeleaje, Wilson anaishia kuguna na kutikisa kichwa kwa shida, ikiwa ni ishara ya kuitikia salamu yangu.
Hilo tu linathibitisha mateso ya takribani miezi sita ambayo amekuwa akiyapata mtoto huyu, na muda wote huo akiwa mtu wa kitandani kinyume na watoto wenzake huko nje wanaokwenda, shule, kusoma na kucheza ambao miezi sita iliyopita alikuwa akijumuika nao pamoja. Pembeni mwa godoro alilolalia Wilson, amelala mama yake aitwaye Neema.
Mama huyu anasema amelala pale kutokana na shinikizo la damu (pressure) linalomsumbua.
"Tangu jana nasumbuliwa na presha," anasema Neema akiwa ameketi kwenye godoro, kando ya mwanawe. Maneno machache yanayoweza kumwelezea kwa kifupi mtoto Wilson ni kwamba hawezi kuamka kitandani, hajigeuzi na hata matumaini ya kurejea shuleni sasa kwake yanaonekana kama miujiza.
Kilichomfanya mtoto huyu awe hivyo ni ajali. Masimulizi yanaonesha kwamba siku ya tukio, Wilson akiwa amepakiwa kwenye pikipiki, waligongwa na gari ina ya Fuso katika eneo la Mpiji Magowe.
Mbali na kuvunjika mguu, mtoto huyo wa nne kati ya watoto sita wa Jackson Ngowo, alipata pia matatizo kwenye kichwa na ubongo kutokana na ajali hiyo.
Ufafanuzi zaidi wa wazazi wake wakimkariri daktari wa mtoto huyo na vipimo vya X-ray unaonesha kwamba mishipa inayounganisha kichwa na uti wake wa mgogo iliathiriwa na hivyo kuathiri pia uwezo wake wa kutoa sauti.
Kwa mujibu wa wataalamu (angalia katika www.asha.org), Wilson atakuwa pia anasumbuliwa na tatizo linaloitwa kwa Kiingereza aphasia linalomfanya ashindwe kuzungumza. Hii ni hali ya mtu kushindwa kuongea kutokana na sehemu ya ubongo wake, hususani nusu ya ubongo wa sehemu ya kushoto, kupata majeraha.
Mtandao huo pia unaonesha kwamba mtu mwenye aphasia, mbali na kushindwa kuongea, anaweza pia kushindwa kusikia, kusoma na kuandika lakini hilo haliathiri uwezo wake kiakili (intelligence).
Wilson kila mara anaonekana mwenye huzuni hata pale anapotaka kuonesha kufurahia wageni wanaomtembelea. Baada ya kuniona, kwa mfano, alionesha hali ya kutaka kutabasamu, lakini ikawa ngumu kwake kutokana na hali aliyonayo.
Mtoto huyu, kwa sasa anahitaji nepi maalumu aina ya pampas, anahitaji lishe na kubwa zaidi ni matibabu ili aweze kurudi katika hali yake ya kawaida au hata kama hatafikia kwa asilimia 100 basi amudu kujisaidia mwenyewe.
Mkasa wenyewe Masimulizi ya wazazi wake yanaonesha kwamba ilikuwa Jumapili ya Februari 28 mwaka huu, siku iliyobadili utaratibu na ugumu wa maisha wa familia ya Jackson Ngowo na mkewe, Neema Ndosi, pale watoto wao wawili walipopata ajali ya kugongwa na Fuso.
Siku hiyo, baba yao (Jackson) ambaye ni fundi mwashi, aliwatuma wanawe hao, Ibrahim na Wilson kwenda kwenye kibanda cha kutolea pesa ili kumletea fedha taslimu alizokuwa anazihitaji kutoka kwenye simu yake.
“Nilikuwa nimewatuma kutoa fedha kwenye simu. Walipoona kile kibanda nilichowatuma kimefungwa walikwenda kibanda cha mbele zaidi na wakaomba kijana wa jirani awapakize kwenye pikipiki, ndipo walipogongwa na Fuso, anasema Ngowo ambaye sasa anaishi Goba alikosaidiwa kupanga vyumba viwili. Anaongeza: “Baada ya wanangu kupata ajali, nilipigiwa simu kuwa mwanao mmoja amefariki dunia (Wilson) na mwingine hali ni mbaya (Ibrahim)."
Anasema aliwakimbiza watoto wake hao wawili kwenye hospitali ya Tumbi, Kibaha baada ya kugundua kwamba hata Wilson alikuwa hajafa.
Anasema kutokana na hali yake, baadaye Wilson alihamishiwa kwenye Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambako alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa miezi mwili na siku tisa.
“Hali imekuwa ngumu kwangu kwa miezi sita yote ya kuuguza wanangu wawili. Mmoja alikuwa amelazwa Tumbi, Kibaha na mwingine ICU, Muhimbili kwa miezi miwili na siku tisa,” anasema.
Kama ilivyo kawaida kwa ajali nyingi, Ngowo anasimulia kwamba Fuso lililosababisha ajali hiyo na kukatisha ghafla furaha na ustawi wa Wilson lilikimbia na hawakuweza kulitambua.
Mama wa watoto hao, Neema anasema wamehangaika sana kuokoa maisha ya watoto wao na hivyo anawashukuru majirani na wasamaria waliowasaidia hadi kufikia hapo. Hata hivyo, anasema hali bado imekuwa nzito katika kuwauguza watoto wao, hasa Wilson kutokana na gharama nyingi kuhitajika kulinganisha na uwezo wao.
“Tulilazimika kuuza makochi, vitanda na magodoro, nguo na vitu vidogo vidogo ili kuweza kugharamia matibabu ya watoto wetu.
“Hata haya magodoro tuliyonayo sasa tumepewa na wasamaria wema na hata vyumba hivi viwili tulivyopanga ni hisani ya watu," anasema. Ngowo anaomba watanzania kusaidia matibabu ya mtoto wake Wilson.
“Nashukuru Mungu kwa Ibrahim afya yake imetengamaa lakini kwa Wilson hali bado ni mbaya kwani ni mtu wa kujisaidia kila kitu na hajaweza kurejea katika hali ya kawaida,” anasema.
Ngowo anasema gharama za matibabu ya mtoto wake ambaye sasa anamtibu katika hospitali ya Profesa William Matuja iliyopo Upanga ni wastani wa Sh 200,000 hadi Sh 400,000 kwa mwezi, na kwamba matibabu hayo yanatakiwa kuchukua zaidi ya mwaka mmoja.
“Tuliporuhusiwa MOI, hali ya mtoto haikuwa si ya kuridhisha kabisa, tuliruhusiwa tukiwa bado tunamlisha kwa mipira, lakini baada ya kumpeleka kwa Profesa Matuja, ndio unafuu ambao kwa sasa tunaona kwa mwanetu. Sasa anaweza hata kuguna unapowasiliana naye,” anasema Ngowo.
Ukiachia gharama za matibabu ambazo ni kumuona daktari na dawa, lakini pia Wilson anatakiwa kufanyiwa usafi wa kidonda kila baada ya siku mbili au tatu, matibabu yanayogharimu zaidi ya Sh 22,000 pamoja na usafiri.
“Kwa hali yake, huwezi kumsafirisha kwa bodaboda wala bajaji, hivyo tunalazimika kutumia gari ili aweze kulazwa kwenye kiti, jambo ambalo linachangia gharama hiyo," anasema. Anasema kilichobainishwa na daktari ni kuwa misuli inayounganishwa kichwa na uti wa mgongo ndiyo iliyoathirika sambamba na mfumo wa sauti ingawa uti wa mgongo haujapata matatizo.
Ngowo anasema alipewa barua ya kutakiwa kwenda hospitali ya Jeshi ya Lugalo kwa ajili ya kumfanyia mazoezi ya misuli lakini huko akajibiwa kuwa hospitali hiyo inaweza kumfanyisha mazoezi tu mtoto ambaye anaweza kutembea au kujitegemea. Anasema huko walimtaka ampeleke katika hospitali ya Mbweni ambayo gharama yake ni Sh 25,000 kila anapofanywa mazoezi.
Anasema wapo hata waliomwambia tatizo la Wilson, linaweza kutibiwa kirahisi nje ya nchi, hususani India, lakini hilo hataki kulifanyia kazi kwa sasa kwani ni 'mlima mkubwa' kwake kama tu matibabu ya hapa ndani inakuwa shida.
“Kusema ukweli nimekwama kabisa ndio maana nimekuja kwenu, ili kupitia ninyi (waandishi wa habari) niwaombe watanzania wanisaidie kunusuru maisha ya mwanangu. Natamani arudi tena shule na kuendelea na masomo,” anasema.
Anaongeza: “Hata tuliporuhusiwa kutoka Moi nilikuwa na deni la zaidi ya laki saba, ambalo wasamaria wema ndio walionisaidia kulilipa."
Kutokana na hali ya maisha ya familia yake, hata suala la lishe kwa mtoto huyo bado linaonekana gumu, jambo ambalo linazidi kudhoofisha mwili wa Wilson na hivyo kuchelewesha uponyaji kwake.
Neema anasema kwa mujibu wa maelekezo ya daktari mtoto huyo anatakiwa kunywa lita moja ya maziwa kila siku, uji wa lishe na samaki aliyechemshwa na supu ya mboga, vyakula ambavyo vitamsaidia pia katika kupona haraka.
“Kutokana na hali yetu hakuna hata tunachokifuata. Tumekuwa tukimlisha chochote kinachopatikana, hasa uji pale tunapojaliwa kupata fedha,” anasema huku akiwa anamlisha uji wa sembe unaoaminika kwamba hauna virutubisho vya muhimu mwilini kwani unatokana na unga wa kukoboa.
Aidha, Ngowo pia anaomba jamii ya watanzania imesaidie kupata kiti cha magurudumu kitakachosaidia kumkalisha mtoto huyo ili kunyoosha viungo, tofauti na sasa ambapo muda mwingi amekuwa akilala.
“Muda mwingi amekuwa akilala, mara moja moja namtoa nje kwa kumbeba ili aote jua, maana daktari alituelekeza kuhakikisha tunamtoa nje,” anasema Neema.
Anaongeza: “Hata wakati wa kumsafisha inakuwa shida. Ni lazima nimvute mbele na kisha nimgeuze taratibu upande mmoja na upande mwingine, hali ambayo inamuongezea maumivu." Familia ya Ngowo inaomba msaada wa hali na mali ili kusaidia matibabu ya mtoto wao Wilson Jackson.
Mnaombwa msaada kupitia simu namba 0652 255 942 (Jackson Ngowo) au 0742 731 878 (Neema Ndosi). Aliyeguswa pia anaweza pia kumchangia chochote mtoto huyu kupitia Mhariri wa gazeti la Habari leo 0766 843 3
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni