Jumatatu, 21 Novemba 2016

Mchungaji apulizia waumini Doom Afrika Kusini akidai ni tiba

  Lethebo Rabalago akimpulizia muumini Doom
MOUNTZION GENERAL ASSEMBLY 
Lethebo Rabalago anadai dawa ya Doom inaweza kuwaponya watu saratani na HIV
Mchungani wa Afrika kusini ambaye aliwapulizia dawa ya kuua wadudu inayoitwa Doom waumini amelaaniwa vikali.
Katika taarifa aliyoituma kwenye ukurasa wa Facebook, mchungaji aliyejitangaza kama nabii Lethebo Rabalago alidai dawa ya kuua wadudu inayojulikana kama Doom inaweza kuwaponya wengi.
Kampuni inayozalisha Doom imeonya juu ya hatari ya kupuliza dawa hiyo watu, huku tume maalum ya serikali ikimtaka yoyote atayeathirika kuwasilisha malalamiko.
Lakini mchungaji huyo ametetea kitendo hicho, akiiambia BBC kuwa anatumia mbinu zisizo za kawaida kuwaponya watu.

Muumini akipulizwa dawa ya Doom
Mchungaji anadai waumini wamekuwa wakipona kwa kupulizwa dawa ya Doom 
 
Nchi hiyo imekuwa na wimbi la visa ambapo wajumbe wa kanisa wamekuwa wakitendewa vitendo visivyo vya kawaida ili kupata tiba.
Katika picha zilizosambazwa kwenye kurasa za Facebook na Twitter, Bwana Rabalago, anayeendesha kanisa la Mount Zion General Assembly katika jimbo la Limpopo, anaeonekana akimpulizia mgonjwa dawa ya kuua wadudu moja kwa moja kwenye macho yake na maeneo mengine mbali mbali ya mwili mbele ya waumini wa kanisa lake.

'Nguvu za Mungu'

Amemueleza mwandishi wa BBC Nomsa Maseko aliyeko mjini Johannesburg kwamba alipuliza dawa hiyo kwenye uso wa mmoja wa wanawake kwa sababu alikuwa na maambukizi ya macho na kudai kuwa "yuko sawa kwa sababu anaamini nguvu za Mungu".
Pia alidai kuwa dawa hiyo ya Doom inaweza kuponesha saratani na virusi vya HIV vinavyosababisha UKIMWI..
Kampuni inayotengeneza dawa ya Doom kwa nembo ya Tiger inasema kuwa inamsihi mchungaji aliyejitangazia kuwa ''nabii'' huko Limpopo - Lethebo Rabalogo kuacha kuwapuliza dawa ya wadudu kwenye nyuso za binadamu kama sehemu ya imani ya kuabudu:
 
Kopo la Doom
  Kampuni ya Tiger iko katika mchakato wa kuwasiliana na Nabii kumtaka aache kufanya tendo hilo
''Tunaona tendo hili kuwa kutia hofu kubwa , na tungependa kubainisha wazi kwamba ni hatari kupulizia Doom ama dawa nyingine yoyote ile ya wadudu kwenye macho ya watu''.
''Doom ilitengenezwa kwa ajili ya kuwaua wadudu wa aina fulani ambao wameonyeshwa kwenye kopo, na maelezo yaliyoandikwa bayana kwenye kopo la Doom yameonya juu ya hatari na yanapaswa kufuatwa.''
''Kampuni ya Tiger iko katika mchakato wa kuwasiliana na Nabii kumtaka aache kufanya tendo hilo,'' imesema kampuni ya Tiger.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni