Jumatatu, 21 Novemba 2016

Watu 16 wauawa kwa sababu ya nyani nchini Libya

Nyani

Ghasia ziliibuka baada ya nyani anayemilikiwa na mtu wa kabila moja kushambulia kundi la wanafunzi wa kike wa kabila jingine.
Maafisa na wanaharakati nchini Libya wanasema kwamba makabiliano mabaya baina ya makabila yameanzishwa na nyani mdogo. Taarifa haziko wazi zote, lakini duru kutoka katika mji wa kusini wa Sabha zinasema kuwa ghasia ziliibuka baada ya nyani anayemilikiwa na mtu wa kabila moja kushambulia kundi la wanafunzi wa kike wa kabila jingine.
Taarifa moja kutoka shirika la habari la AP inasema kuwa vijana watatu walimkimbiza nyani wakimuelekeza kwa msichana wa shule ya sekondari wiki iliyopita, na kumjeruhi msichana huyo.
Familia ya msichana huyo ilitaka kulipiza kisasi baada ya nyani kumkwaruza na kumpiga ndipo walipowauwa vijana wote watatu pamoja na nyani wao.
Tukio hilo liliibua mauaji ya ulipizaji kisasi, ambayo yamesababisha mapigano ya siku nne. Takriban watu 16 wameripotiwa kufariki dunia na wengine makumi kadhaa kujeruhiwa.
Makabila makuu ya Sabha, Awlad Suleiman na Gadhadhfa, kila moja linaungwa mkono na makundi yenye silaha, linaripoti shirika la habar la AP.
Libya iliingia katika ghasia baada ya mtawala wake wa muda mrefu Kanali Muammar Gaddafi kupinduliwa na kuuawa mnamo mwaka 2011. Eneo kubwa la nchi kwa sasa linatawaliwa na makundi ya wanamgambo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni