Jumanne, 3 Januari 2017

Bonge mwenye kilo 590 kukata nusu ya uzito

Bwana mmoja mwenye unene wa kilo 590 nchini Mexico amepanga kupnguza nusu ya uzito wake ifikapo mapema mwakani kwa lengo la kuinusuru afya yake ambayo umekuwa ikizorota kwa maradhi.
Mmexico huyo anayeminika kuwa mtu mwenye uzito mkubwa kabisa duniani, Juan Pedro, atafanyiwa upasuaji katika kipindi cha mwaka mpya ujao na kupunguza uzito wake kwa takribani nusu. Daktari wake, Jose Castaneda Cruz, amesema Pedro, mwenye uzito wa kilo 590 na anayekabiliwa na kisukari, shinikizo la damu na tatizo sugu la kupumua, anahitaji kupunguza uzito wake, kwa lengo la kuondosha athari za kiafya. Amesema mgonjwa wake huyo atapaswa kupitia hatua kadhaa kabla ya kufikia utaratibu kamili wa upasuaji, ambapo mchakato wake utatekelezwa katika hatua mbili ili kuweza kukabiliana na hatari kubwa za kiafya anazokabiliana nazo.
Matibabu kamili

Pedro ataondolewa zaidi ya robo tatu nyama za tumboni. Na sehemu nyingine ya tumbo itazibwa ili kumweka sawa. Aidha dokta huyo amesema atafanyiwa Upasuaji wa tumbo, kwa sehemu ya ndani. Daktari Castaneda anataka mgonjwa wake apunguze kilo 59 katika kipindi cha miezi sita ijayo, ambapo kwa kiwango hicho tu, anaweza kupunguza unene uliokithiri unaoweza kusababisha saratani kwa asilimia 52. Duru za kitabibu zinasema kwa ujumla, Juan Pedro mwenye umri wa miaka 32 ana fursa nzuri ya kupunguza nusu nzima ya uzito wake baada ya upasuaji wa kwanza katika kipindi cha miezi sita. Mwenyewe amenukuliwa akiwaambia waandishi wa habari "Taratibu lakini kwa uhakika, itafikia lengo".

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni