Na AGATHA CHARLES-
DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, amethibitisha kujiuzulu kwa Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Gabriel Mnyele.
Kupitia taarifa yake iliyoandikwa kwa kifupi na kutumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Msigwa, hakutaja sababu ya Mnyele kuomba kujiuzulu bali alisema: “Ombi la Mnyele aliyeomba kujiuzulu wadhifa wake wa Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora limekubaliwa na Rais Dk. John Magufuli. Nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora itajazwa baadaye.”
Taarifa hiyo ya Ikulu ilitumwa jioni ya jana wakati asubuhi yake Mnyele alikuwa tayari ameshaondoka katika kituo chake cha kazi cha Uyui na kuja Dar es Salaam.
Gazeti hili lilipata taarifa na baadaye kuthibitishwa na Mnyele mwenyewe kwa njia ya simu kuwa alikuwa yuko safarini akitoka mkoani humo na angefika Dar es Salaam jana jioni akitumia usafiri wa ndege.
Alitoa taarifa hizo alipozungumza na gazeti hili saa tano asubuhi alipokuwa uwanja wa ndege akisubiri kupanda ndege na kumtaka mwandishi amtafute baada ya saa 10 jioni.
“Tayari niko Dar es Salaam nimeshatoka Uyui, huko nitarudi kukabidhi mwenzangu atakapoteuliwa,” alisema Mnyele.
Gazeti moja marufu nchini lilipotaka kujua sababu za kuchukua uamuzi huo, alisema ulikuwa ni uamuzi binafsi na alimweleza Rais Magufuli hivyo hawezi kuutaja hadharani.
“Uamuzi wa mteuliwa na anayeteuwa ni privacy (siri), hizo ni sababu binafsi, mimi au rais hawezi kuweka hadharani,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni