Wazazi hao wenye hasira walimdhalilisha mwalimu huyo kwa kumcharaza fimbo wakimtuhumu kuwaadhibu watoto wao kwa kuwabebesha matofali bila idhini yao ambapo wamemsababishia maumivu makali mwilini. Shule ya Msingi Kipanga iko katika kata ya Samazi mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika wilaya ya Kalambo.
Binyura alilazimika kuitisha kikao kilichowashirikisha wenyeviti wa vijiji , walimu na watendaji waliopo katika katika kata hiyo ambapo aliagiza wote waliotenda uhalifu huo wasakwe, wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria pamoja na kuagiza mwalimu huyo ahamishiwe kwenye shule nyingine wilayani humo.
Alisema mwalimu huyo ana uwezo wa kufanya kazi sehemu yoyote wilayani humo huku akilaani kitendo alichofanyiwa na wazazi ambacho ni cha udhalilishaji huku akiwataka wananchi na wazazi kuachana na tabia ya kuwadhalilisha walimu.
Mashuhuda walidai kuwa wazazi hao wenye hasira wakiwa na fimbo mikononi mwao walifika shuleni hapo hivi karibuni ambapo walimcharaza fimbo mwalimu huyo sehemu mbalimbali za mwili wake huku tukio hilo likishuhudiwa na wanafunzi wake pamoja na walimu wenzake.
Akizungumzia kisa hicho, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Enock Majenga alisema baadhi ya wakazi wakiwemo wazazi walighadhabishwa na uamuzi na mwalimu Mkalambosa kuwaadhibu wanafunzi ambao hawakushiriki kusogeza matofali kwenye eneo ambalo choo cha shule hiyo kinajengwa.
Aliongeza kuwa mwalimu Mkalambosa wakati shule inafungwa aliwaagiza wanafunzi wawe wanafika shuleni hapo kwa ajili ya kusomba matofali na kuyapelekea eneo la ujenzi wa choo cha shule hiyo ambapo baadhi ya wanafunzi walikaidi na kutohudhuria.
Baada ya likizo kumalizika na shule kufunguliwa mwalimu Mkalambosa aliamua kuwaadhibu wanafunzi wote ambao walishindwa kufika shuleni hapo wakati wa likizo ambapo aliwaamuru kusomba matofali na kuyapekeleka kwenye eneo la ujenzi wa choo shuleni hapo.
“Ghafla kundi la wananchi, wengi wao wakiwa wazazi wa wanafunzi hao walifika eneo la shule na kumvamia mwalimu huyo na kuanza kumcharaza fimbo na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake,” alieleza.
Ofisa Elimu wa Kata ya Samazi, Daudi Sengo alikiri kutokea kwa mkasa huo ambapo ameshatoa taarifa wilayani akisisitiza kuwa mwalimu huyo amehamishiwa katika Shule ya Msingi Mbuza iliyopo wilayani humo .
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni