Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Ramo Makani
SERIKALI imesema itaimarisha utalii wa misitu ya asili nchini utoe
mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa tofauti na ilivyo hivi sasa
inapotegemea zaidi utalii wa wanyamapori.Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani (pichani) amesema hayo wilayani Lushoto mkoani Tanga jana wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja kutatua migogoro mbalimbali ya uhifadhi.
Alisema sekta ya utalii nchini imekuwa ikitegemea sana wanyamapori na kusahau vivutio vingine kama vile misitu ya asili ambayo ndani yake kuna mimea na viumbe hai mbalimbali adimu duniani na ambavyo hupatikana Tanzania pekee.
“Tumezoea zaidi utalii wa wanyamapori, utalii wa misitu unaweza kuzidi hata wa wanyamapori, kwenye misitu yetu ya asili tunajivunia mimea adimu ya asili na viumbe hai mbalimbali kama vile ndege, vyura, vipepeo, mijusi na kadhalika, tunachotakiwa kufanya ni kutunza misitu yote ya asili, tuiboreshe na kuitangaza ili kupata watalii wengi zaidi na Pato la Taifa liendelee kukua,” alieleza.
Kwa mujibu wa tovuti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina jumla ya hifadhi za misitu ya asili 100, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na hifadhi za taifa ambazo zipo 16 pekee.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni