Alhamisi, 10 Agosti 2017

Mwanamume apatikana akisafirisha mikono ya binadamu China

Mkono ulivyoonekana kwenye mtambo wa usalama
Maafisa wa usalama kusini magharibi mwa China walipigwa na butwaa hivi majuzi walipogundua mwanamume mmoja alikuwa akisafirisha mikono miwili ya binadamu.
Kwa mujibu wa Pear Video, mzee wa miaka 50 kwa jina Zheng alisimamishwa na maafisa wa polisi katika kituo cha mabasi cha Duyun, katika mkoa wa Guizhou baada ya mikono miwili ya binadamu kugunduliwa na mtambo wa kiusalama tarehe 31 Julai.
"Nilimuuliza alikuwa amebeba nini kwenye mkoba wake, na akanijibu kwamba ulikuwa ni mkono," afisa wa usalama aliambia Pear Video.
Kwa mujibu wa gazeti la South China Morning Post, alizuiliwa mara moja, wakimshuku kuwa huenda alikuwa amehusika katika mauaji.

Hata hivyo, Bw Zheng aliwafafanulia kwamba alikuwa akisafirisha viungo hivyo kwa kakae, ambaye alikuwa amekatwa mikono baada ya kuhusika katika ajali ya mtambo wa umeme.
Bw Zheng alisema kakake aliomba asaidiwe kusafirisha mikono hiyo hadi alikokuwa akiishi, ili atakapofariki, mwili wake na viungo hivyo, vizikwe eneo moja.
  China
Huwa kawaida kwa wasafiri kukaguliwa wakiwa vituo vya mabasi China
Bw Zheng aliachiliwa huru na maafisa wa serikali baada ya hospitali iliyokuwa ikimtibu kakake kuthibitisha kisa hicho.
Nchini China, watu huamini kwamba mwili unafaa kuchomwa ukiwa mzima au kuzikwa pia ukiwa mzima ndipo marehemu awe na amani.
Hata hivyo, wengi wa waliosoma taarifa hiyo mtandaoni wameshangazwa sana na kisa hicho, ikizingatiwa kwamba maafisa wa matibabu huhitaji kibali maalum kuruhusiwa kusafirisha viungo vya binadamu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni