Mpigapicha mmoja
ameshinda kesi iliyodumu kwa miaka miwili dhidi ya kundi la kutetea haki
za wanyama kuhusu haki za kumiliki picha ambayo ilipigwa na tumbili.
Tumbili
kwa jina Naruto alidaiwa kujipiga picha hiyo katika msimu mmoja
Indonesia mwaka 2011 alipoichukua kamera iliyokuwa inamilikiwa na David
Slater kutoka Monmouthshire.Majaji nchini Marekani wamesema tumbili huyo hangekabidhiwa haki miliki ya picha hiyo.
Watetezi wa haki za wanyama kutoka kwa kundi la People for the Ethical Treatment of Animals (Peta), ambao walikuwa wamewasilisha kesi hiyo kwa niaba ya tumbili huyo, walisema mnyama huyo anafaa kufaidi kwa njia fulani.
Kesi hiyo ya Peta "kwa niaba ya tumbili" imetupiliwa mbali lakini Bw Slater amekubali kutoa asilimia 25 ya mapato yatakayotokana na picha hiyo siku zijazo.
Kwenye taarifa ya pamoja, Peta na Bw Slater, wamesema mpiga picha huyo atatoa robo ya pesa atakazopata kupitia uuzaji wa selfie za tumbili huyo kwa mashirika ya hisani yaliyosajiliwa "ambayo yamejitolea kulinda maslahi au makazi ya Naruto".
"Kesi hiyo ya Peta ilikuwa imezua mjadala mkubwa kimataifa kuhusu haki za kimsingi za wanyama kwa jumla, na si zaidi kwa jinsi wanavyotumiwa na binadamu kujifaidi," wakili wa Peta, Jeff Kerr amesema.
Bw Slater, kutoka Chepstow, alikuwa amejitetea kwamba anafaa kuimiliki picha hiyo akisema alifanya juhudi sana kabla ya kuipata picha hiyo.
Alisema juhudi zake hazingeweza kulipwa hata kwa kudai hakimiliki pekee.
Bw Slater akijitetea alisema ilimchukua siku tatu za 'kazi ngumu' kupata picha hiyo. Alisema pesa zinazotokana na kutumiwa kwa picha hiyo, aliyoipiga katika kisiwa cha Sulawesi nchini Indonesia mwaka 2011, ni zake.
"Ilinichukua siku tatu za kutoa jasho kupata selfie hii kuhakikisha ninakubalika na kundi la kima kabla yao kunikubali kiwakaribie vya kutosha na kuwaonyesha kamera yangu," Bw Slater aliambia BBC mwaka 2015.
"Tatizo ni kwamba, watu wengine wanajaribu kuiba haki zangu za umiliki na nitapinga hilo."
Selfi hiyo ilisambazwa sana kote duniani na mtandaoni. Waliompinga Slater wanasema hawezi kuwa na hakimiliki ya picha hiyo kwa sababu ilipigwa na mnyama.
Kesi hiyo ilikuwa imeorodheshwa kama "Naruto v David Slater" lakini kulikuwa pia na mzozo kuhusu utambulisho wa tumbili aliyehusika.
Peta walidai alikuwa tumbili jike kwa jina Naruto lakini naye Bw Slater akadai alikuwa tumbili tofauti wa kiume.
Lakini majaji wa mahakama ya rufaa mjini San Francisco wamekubali hoja za Bw Slater baada ya vuta nikuvute ya miaka miwili mahakamani.
Taarifa ya pamoja ya Peta na Bw Slater imesema kesi hiyo "iliibua masuala muhimu kuhusu kupanuliwa kwa haki za kisheria kwa wanyama, ambao si binadamu".
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni