Kutokana na tukio hilo, mtoto huyo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Isinde Kata ya Mtapenda katika Halmashauri ya Nsimbo wilayani Mlele mkoani Katavi, amelazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda kwa matibabu baada ya simba huyo kumjeruhi vibaya paja lake la mguu wa kulia.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, Dk Theopister Elisa amethibitisha kuwa mtoto huyo amepokelewa na kulazwa hospitalini hapo kwa matibabu, akiwa amejeruhiwa paja lake la mguu wa kulia.
Akisimulia mkasa huo, mtoto huyo alisema kuwa usiku huo wa tukio alikuwa amelala fofofo pembeni mwa zizi la ng’ombe lililopo nyumbani kwao, lakini alishtuka ghafla usingizini baada ya kuhisi kuwa alikuwa akipapaswa mwilini na mnyama.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Madirisha Lubinza ambaye pia anafuga mbwa wengi kwa ajili ya ulinzi, alieleza kuwa usiku wa tukio hilo alisikia kelele za mtoto wake akiomba msaada huku simba akiunguruma kwa nguvu, ambapo alitoka nje ya nyumba yake. Alidai aliwaita na kuwaamuru mbwa wake, wamshambulie simba huyo ndipo walipoanza kumbwekea na kumtisha na baadaye simba huyo aliingiwa hofu na kukimbilia porini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni