Ijumaa, 8 Desemba 2017

Bitcoin yagonga $17,000 huku wasiwasi ukizidi

Bitcoins and dollar notes

 Thamani ya Bitcoin imepanda sana wiki za karibuni
Thamani ya sarafu ya dijitali ya Bitcoin ilifikia $17,000 (£12,615) katika masoko barani Asia, na kuendeleza mtindo ambao umekuwa ukishuhudiwa siku za karibuni.
Sarafu hiyo imeongezeka thamani 70% wiki hii kwa mujibu wa Coindesk.com, licha ya tahadhari kutolewa kwamba huenda uwekezaji katika sarafu hiyo ukawa "puto hatari".
Kupanda thamani kwake kumefananishwa na "treni inayoongeza kasi zaidi na zaidi ilhali haina breki".
Huku wasiwasi ukiongezeka, kundi moja limeonya kwamba mpango wa kuanzisha masoko ya fedha za bitcoin hameharakishwa.
Katika masoko ya barani Asia, sarafu hiyo ilipanda sana kabla ya kushuka kiasi na kutulia katika $16,000.
 Wakosoaji wa fedha hizo wamesema kupanda thamani kwake kwa sasa ni "puto hatari" kama ilivyofanyika kwa dotcom, lakini wengine wanasema kupanda bei kwake kunatokana na kuanza kukubalika kwa fedha hizo.
"Bitcoin kwa sasa ni kama treni inayoongeza kasi zaidi na zaidi ilhali haina breki," amesema Shane Chanel wa shirika la kifedha la ASR Wealth Advisers la Sydney.
Kupanda thamani kwa Bitcoin kumechangiwa pia na masoko ya fedha za aina hiyo ambayo yanatarajiwa kufunguliwa wikendi hii.
Bitcoin itaanza kuuzwa katika soko la Cboe Futures Exchange mjini Chicago Jumapili na baadaye, soko kubwa la ubadilishanaji wa fedha kama hizo la CME litaanza kuuza fedha hizo wiki moja baadaye.
Ingawa watu wengi wamewekeza mabilioni ya dola katika Bitcoin, thamani ya jumla ya $268bn ya fedha hizo kwa jumla bado ni ndogo ukilinganisha na aina nyingine za mali au fedha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni