Jumamosi, 25 Januari 2014

MAFURIKO KILOSA MTU MMOJA ANUSURIKA KIFO

Mkulima mkazi wa kijiji cha Magole, wilayani hapa, amenusurika kifo baada ya kusombwa na mafuriko umbali wa meta 225 akiwa shambani eneo la Feri Magole na kunasa kwenye mti wa myegeya na kuning'inia kwa saa saba.
Khatib Bakari (30), ambaye mara nyingi hushinda shambani akilima na kulinda mazao yake hasa mahindi mabichi na minazi, siku hiyo alilala kibandani kwenye mashamba ya ndugu zake na kukutwa na majanga hayo usiku wa manane wa kuamkia Januari 22.
Baada ya kubainika amesombwa na mafuriko na kunasa kwenye mti na kujiokoa alfajiri, mamia ya wananchi wa kijiji cha Magole, walifika eneo hilo kumshuhudia mwenzao huyo akiwa mtini bila nguo ambazo maji ya mafuriko yalimchojoa.
Hata hivyo, baada ya kuona umati wa watu ukimwangalia alijificha kwenye matawi ili kujisitiri ingawa alikuwa umbali mrefu kutoka barabara ya Magole - Turiani.
Mwandishi wa habari hizi na viongozi wa serikali ya wilaya ya Kilosa na Mkoa wa Morogoro, akiwamo Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera, na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, walimwona mtu huyo akiwa mtini huku chini maji yakipita kwa kasi.
Hata hivyo, viongozi hao akiwamo Mkuu wa Mkoa, walitoa ushauri wa kutafuta namna ya kumwokoa baada ya kukaa mtini kwa saa nyingi.
Kutokana na mwito huo, watu 18 walijitokeza na kamba na madumu matupu ya plastiki, kwenda kumwokoa ambapo walipiga mbizi na kumfikia na kufanikiwa kumwokoa majira ya saa 9 alasiri baada ya saa mbili za kazi.
Akizungumza baada ya kuokolewa, Bakari alimshukuru Mungu kwa kumlinda, pia wanakijiji wenzake waliojitokeza kumwokoa juu ya mti katikati ya mafuriko.
"Maji yalifika eneo la kibanda changu saa saba usiku nimelala, nilishituka maji yamejaa na kukosa sehemu ya kupita, nikasombwa umbali wa ekari tatu za shamba, Mungu ni mkubwa, nilinasa kwenye mizizi ya mti wa myegeya, nikapanda juu bila nguo - zilichojolewa na maji," alisema kwa masikitiko.
Bakari ambaye hana mke wala mtoto, alisema anaishi na ndugu zake kijijini hapo na shughuli zake ni kilimo, hivyo mara zote hushinda shambani.
Juzi baada ya maji kupungua, wananchi walikuwa katika hekaheka za kusafisha na kutoa mabaki ya maji na taka kwenye nyumba zao, na wengine kwenye nyumba za ibada ukiwamo Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Magole

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni