JELA KWA MIAKA 65 KWA KUMPA UJAUZITO MTOTO WAKE WA KUMZAA.
MKAZI wa Mtaa wa Uhamila katika mji mdogo wa Rujewa,
mkoani Mbeya, amehukumiwa miaka 65 jela kutokana na makosa matatu tofauti,
yaliyotokana na kumpa ujauzito mwanawe wa kumzaa.
Mahakama ya Wilaya ya Mbarali
mkoani Mbeya ilitoa hukumu hiyo jana kwa Benjamin Muyinga (48) baada ya kutiwa
hatiani kwa makosa hayo.
Hakimu Mfawidhi Kinabo Minja alimhukumu
mshitakiwa kutumikia jela miaka 30 kwa kosa la kufanya mapenzi na mtoto wake,
miaka 30 mingine kwa kubaka mtoto wake na miaka mitano jela kwa kumpa mimba
mwanafunzi.
Minja alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani
hapo hivyo atatumikia adhabu hiyo kwa pamoja kwa maana kwamba atakaa jela miaka
30.
Mashitaka yaliyokuwa yakimkabili mahakamani hapo ni kufanya mapenzi
na mtoto wake, kubaka mtoto wake na la tatu ni kumpa mimba mwanafunzi.
Awali ilidaiwa mahakamani na Mwendesha Mashitaka wa jeshi la Polisi,
Mazoya Luchagula, mbele ya Hakimu Mfawidhi Kinabo Minja, Oktoba 18 mwaka jana,
mwanafunzi (jina linahifadhiwa) aliyekuwa na umri wa miaka 14, alikuwa mjamzito.
Luchagula alidai walimu wa shule hiyo ndiyo walitilia shaka suala la
mwanafunzi huyo aliyekuwa darasa la tano katika shule ya msingi iliyoko Rujewa
kwamba alikuwa na ujauzito. Alipelekwa hospitali na kwenda kukutwa akiwa na
mimba ya miezi minne.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka, baada ya
kuhojiwa, mwanafunzi huyo alidai ujauzito ulikuwa wa baba yake mzazi waliyekuwa
wakiishi naye wawili nyumbani kutokana na baba yake kutengana na aliyekuwa mkewe
ambaye hivi sasa anaishi jijini Mbeya.
Mwanafunzi huyo alibainisha namna
alivyokuwa akiishi na baba yake baada ya wazazi wake kutengana na kwamba
alimgeuza ‘mkewe’ kwani alikuwa akilala naye na kufanya naye mapenzi hadi
ilipobainika kuwa na ujauzito huo.
Katika kile kilichoelezwa na upande
wa mashitaka kwamba kitendo kilichofanywa na mzazi huyo hakikubaliki katika
jamii ya Watanzania, Mwendesha Mashitaka aliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa
mshitakiwa iwe fundisho kwake na wazazi wengine wenye tamaa zenye kusababisha
ukatili dhidi ya watoto wao. HABARILEO (TK)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni