Wawakilishi wa Chama cha Uhifadhi wa Wanyama cha Frankfurt (FZS), wakikabidhi magari zaidi ya 11 kwa Rais Jakaya Kikwete Ikulu Dar es Salaam jana, kwa ajili ya kusaidia vita dhidi ya ujangili wa wanyamapori katika hifadhi na mbuga za taifa. Picha na Ikulu
Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali imenuia kumaliza kabisa ujangili nchini, ikiwa ni hatua ya kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka katika hifadhi za taifa.
Hakusita kusisitiza kwamba, nia ya dhati ya Serikali ni kuhakikisha mkakati huo unakamilika, japokuwa kumekuwa na changamoto zinazotokana na ukubwa wa hifadhi hizo na uhaba wa vitendea kazi pamoja na askari wa wanyamapori.
Akizungumza wakati wa kupokea magari 11 ya kisasa kwa ajili ya kusaidia operesheni ya kupambana na ujangili kutoka kwa Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) la Ujerumani, Kikwete alisema tatizo hilo limekuwa la muda mrefu, lakini juhudi za kulikomesha zinafanyika.
Alisema, pamoja na ukubwa wa tatizo hilo, bado kuna tatizo la uhaba mkubwa wa wafanyakazi wanaotakiwa kudhibiti majangili, ambapo kwa sasa kuna wafanyakazi 1,155 sawa na asilimia 24 tu ya mahitaji halisi ya wafanyakazi 4,000 wanaohitajika.
"Mwaka uliopita, Serikali ilisimamia ajira ya wafanyakazi 449 na sasa kuna ajira ya wafanyakazi 500.
Kwa maana hiyo tutafikisha wafanyakazi wapya 949 na kufanya mahitaji ya wafanyakazi wapya kuwa 4,000 zaidi ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa viwango vya kimataifa," alisema.
Kwa mujibu wa viwango vilivyopo sasa, mfanyakazi mmoja anasimamia eneo la kilometa za mraba 169 ikilinganishwa na viwango vya kimataifa vya kilometa za mraba 25 kwa kila mfanyakazi mmoja.
Rais Kikwete alisema kwa sasa Serikali itaendelea kuajiri idadi hiyo ya wafanyakazi kila mwaka kwa miaka mitatu ijayo ili kuhakikisha pengo lililopo linazibwa.
Alisisitiza kuwa, kampeni dhidi ya ujangili ni suala la kimataifa na Tanzania au nchi zilizoathirika hazitaweza kulikabili bila ushirikiano wa kimataifa.
Alisema upo ulazima wa kuteketeza mitandao yote ya ujangili na kuwawajibisha ipasavyo watakaonaswa, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kulinda urithi huo wa dunia.
Ukosefu wa vifaa
Akifafanua, Rais Kikwete alisema kuongeza idadi hiyo ya wafanyakazi pekee haitakuwa na maana iwapo hawatakuwa na vifaa maalumu vya kisasa vitakavyowawezesha kukabiliana ipasavyo na tishio la ujangili.
Katika mkakati wa maboresho hayo, Kikwete alisema wanafanya jitihada za kuongeza idadi ya magari, kuongeza vifaa vya kisasa kwa ajili ya doria na vifaa vya mawasiliano, ambavyo vinahitaji uwezo mkubwa wa kifedha ambao utaweza kutekelezwa na serikali kwa kipindi kirefu iwapo haitapata msaada wa uwezeshaji kutoka kwa wadau.
Msimamo wa Wizara
Akizungumzia msimamo na mikakati ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri Lazaro Nyalandu alisema kutokana na ukubwa wa tatizo, wanahitaji vifaa vya kisasa zaidi, ikiwamo helikopta na ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kufanya doria kwenye maeneo yote ya mbuga na hifadhi za taifa.
Aliwatahadharisha wafugaji wanaopenda kuingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi, akiwataka kuondoa mifugo yao mapema kwa kuwa katika operesheni hiyo hakuna atakayeachwa.
"Katika operesheni hii, hakuna jangili wala mfugaji atakayeachwa iwapo atakutwa kwenye maeneo ya hifadhi," alisema.
Alifafanua kwamba, msaada huo wa magari utapelekwa maeneo tofauti, matano kanda nane za Selous, mengine matano Hifadhi ya Serengeti na moja Hifadhi ya Maswa.
Mwaliko wa vyombo vya habari
Nyalandu alisema Wizara yake imevialika vyombo vyote vya habari vya kimataifa kwa ajili ya kuja kupata taarifa sahihi kuhusu kampeni dhidi ya ujangili zinavyotekelezwa ili kuepuka ripoti za upande mmoja kwa ajili ya kuweka usawa.
Alisema hatua hiyo ilichukuliwa na wizara yake walipokwenda kwenye mkutano maalumu na Rais Kikwete ulioandaliwa na mtoto wa Mfalme wa Uingereza, Prince Charles kwa ajili ya kuangalia namna ya kulinda wanyama walio hatarini kutoweka duniani wakiwemo tembo na faru.
Chanzo:Mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni