Jumatano, 16 Aprili 2014

MATUMAINI YA ARSENAL KUCHEZA UEFA YAFUFUKA


MATUMAINI ya Arsenal kufuzu kucheza ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao yameanza kufufuka baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham kwenye mchezo wa ligi kuu soka nchini England uwanja wa Emirates.
Lukas Podolski amefunga mabao mawili katika dakika ya 44 na 78, huku moja likifungwa na Olvier Giroud dakika ya 54.
Westham walikuwa wa kwanza kufunga leo hii katika dakika ya 40 kipindi cha kwanza kupitia kwa Matthew Jarvis .
Mashabiki wa Arsenal huwa hawana imani kubwa na Giroud na katika mchezo wa leo alikosa nafasi kadhaa kipindi cha kwanza, lakini wakati mashabiki wakijiuliza kama mshambuliaji huyo anaweza kuwa tegemeo kwa siku za usoni, alifunga bao muhimu mno katika ushindi huo.
Umuhimu wa bao la Giroud unatokana na uhitaji mkubwa wa Arsenal kufuzu michuano ya UEFA msimu ujao.
Kikosi hicho cha Arsene Wenger kilianza vizuri ligi na kuongoza kwa muda mrefu, lakini mambo yakabadilika ghafla na kuwapisha Chelsea, Man City na Liverpool ambao wanachuana mpaka sasa.
Sasa Wenger na vijana wake wapo katika hatari ya kushindwa kufuzu UEFA kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 17 baada ya kuwapisha Everton katika nafasi ya nne kwa muda.
Lakini baada ya kushinda mechi ya leo dhidi ya wapinzani wao wa London, Arsenal wamerejea nafasi ya nne kwa kufikisha pointi 67, huku Everton wakishuka mpaka nafasi ya tano kwa pointi zao 66, lakini kesho wanacheza dhidi ya Crystal Palace.
Arsene Wenger baada ya mchezo amesema kuwa walikuwa katika presha kubwa ya kushinda mchezo, lakini ilikuwa mechi ngumu mno.
“Niliridhishwa na ukomavu wa timu yangu. Walionesha kutulia baada ya kufungwa bao la kwanza”.


“Kazi kubwa ilikuwa kusawazisha bao kabla ya mapumziko. Ilikuwa vita kubwa na ilikuwa ya kufurahisha”. Alisema Wenger (TK)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni