Bi Kenyatta akilakiwa na mumewe Rais Uhuru
Kenyatta
Mama Margaret Kenyatta mke wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta,
amekuwa mwanamke wa kwanza mama wa taifa kushiriki mbio za London Marathon na
kumaliza mbio hizo.
Alishangiliwa na wakenya wanaoishi nchini Uingereza alipomaliza mbio hizo za
kilomita 42 kwa muda wa saa saba na dakika nne siku ya Jumapili.
Mama Margaret alilakiwa na Rais Kenyatta pamoja na waandalizi wa mbio hizo
mjini London mwishoni mwa mbio huku akiwapa motisha wakenya na jamii ya
kimataifa kwa kuwa mke wa kwanza wa rais kuwahi kushiriki mbio hizo.
Bi Kenyatta alishiriki mbio za London Marathon kama sehemu ya mradi wake wa
kuchangisha pesa za kuwasaidia wanawake wajawazito kujifungua katika mazingira
salama na kuhakikisha kuwa watoto wao pia wanaishi nchini Kenya.
Lengo lake kuu ni kupunguza idadi ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto
wachanga.
Wanawake wengi na watoto wachanga nchini Kenya hupoteza maisha yao wakati wa
kujifungua kutokana na ukosefu wa huduma salama na sasa mama Kenyatta amejitwika
jukumu la kuwapa akina mama wajawazito uwezo wa kujifungua salama.
Bi Kenyatta alikuwa na kikundi cha wasaidizi 8 waliokuwa naye hadi alipofika
mwishoni mwa mbio hizo.
Wakenya kutoka sehemu mbali mbali Uingereza walifika mjini London kushuhudia
Bi Kenyatta akikamilisha mbio hizo.
Wakenya ndio walioshinda mbio hizo upande wa wanawake na wanaume.
Wilson Kipsang aling'aa upande wa wanaume kwa kuweka rekodi mpya ya saa mbili
na dakika nne. Kipsang alifuatiwa na mkenya mwenzake Stanley Biwott.
Kwa upande wa wanawake, Edna Kiplagat alishikilia nafasi ya kwanza akifuatiwa
na mkenya mwenzake Florence Kiplagat
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni